Na Mwandishi wetu
Kwako Raisi Malinzi, ni imani yangu u mzima wa afya na unaendelea vizuri na kazi yako ya ngumu kuiendesha taasisi hii ya soka hapa Tanzania.
Kwa namna ya kipekee nakupa pongezi kwa juhudi zako mbalimbali za kuhakikisha soka letu lina songa mbele na timu ya taifa inafanikiwa.
Pia nakupa pole kwa timu yetu taifa kutolewa na Msumbiji hapo Jumapili. Ni matokeo mazuri kwetu maana ukikosea kitu ndipo wajifunza kujipanga upya na kupata muda wa kujiandaa kwa uzuri zaidi.
Lengo na madhumuni ya kushika kalamu hii ni kutaka kujaribu kupitisha ushauri wangu wa wazi kwako ili niweze kuchangia mambo mawili matatu ya msingi juu ya maendeleo ya soka katika taifa letu kwa ujumla.
Ni dhahiri tumepambana sana kufikia kilele cha mafanikio katika soka lakini tunakwamishwa na vitu vidogo sana haswa katika mipango endelevu ya soka kuanzia vijana wa miaka chini 17 hadi timu ya taifa.
Tulipofikia sasa tumekwama na hatuwezi kuendelea mbele maana tuna tatizo moja kubwa nalo ni kukosa wachezaji wenye umakini wa hali ya juu.
Kupata wachezaji wenye umakini wa hali ya juu si suala la leo wala kesho ni suala linaloweza kutekelezwa kwa mipango endelevu ya muda mrefu na muda mfupi.
Tunajua ili uwe na wachezaji makini ni lazima uwe na ligi bora yenye ushindani wa hali ya juu. Kwa muda mrefu Tanzania tumwekuwa hatuna ligi yenye ushindani wa hali ya juu bali tumekuwa na Ligi yenye timu mbili au tatu ambazo zina ushindani wa kweli.
Hii ndio sababu kubwa inayosababisha timu yetu ya taifa kuyumbaa maana inaundawa na wachezaji wanaocheza soka katika ligi isiyo na ushindani.
Ligi ambayo inachezwa mkoa moja zaidi, ligi ambayo timu inacheza mechi chache za ligi kuliko mechi za kirafiki, Ligi ambayo mapato ya uwanjani ndio yanatumika kusaidia masuala muhimu ya timu.
Najua ni ndoto kuifanya ligi kuwa bora kwa kipindi cha mwaka mmoja na kupata wachezaji bora kutokana na ubovu wa viongozi wengi kwenye vilabu vya ligi kuu, basi ni jukumu lako kuhakikisha timu zote zinakuwa na viongozi bora wa michezo.
Maana hata ligi ikipata wadhamini wa kutosha na vilabu vikawa na pesa za kutoshal akini kama hakuna viongozi wapenda michezo na wenye uchungu na soka la Tanzania basi soka halitasonga mbele kwa namna yoyote.
Lakini jambo kubwa na zuri zaidi kwako mheshimiwa ni kuwekeza katika soka la kulipwa. Kupata wachezaji wengi waocheza soka la kulipwa ndio itakuwa chachu ya ushindi na mafanikio katika timu yetu. Ili timu yetu ya Taifa iwe na mafanikio zaidi tunahitaji huduma za wachezaji wa kulipwa angalau wawili katika kila idara.
Vipaji vipo vingi sana lakini hakuna wa kuviendeleza. Tukipata mabeki wawili wanaocheza soka la kulipwa, wakaja wakasaidiana na wanaocheza soka la ndani nadhani hakutakuwa na magoli ya kizembe. Tukipata viungo wawili wanaocheza soka la kulipwa hakuna shaka tutakuwa na timu nzuri zaidi maana umakini utaongezeka katika kila eneo.
Nakumbuka wakati wa ujio wa Marcio Maximo tulikuwa tuna timu mbovu kuliko maelezo, tulikuwa tunaingia uwanjani kujihami tusifungwe maana kulikuwa na uhaba wa kufunga magoli. Kulikuwa hakuna washambuliaji mahiri wenye kuleta chachu ya ushindani mbele.
Lakini kwa sasa hatuko hivyo, timu yetu inapata magoli mengi na ya kutosha. Katika mechi nne tulizochea zote tumepata magoli lakini Magoli haya yanachangiwa sana na uwepo wa wachezaji wa kimataifa wa Tp Mazembe na hilo lipo wazi halina ubishi.
Mhe Raisi ni jukumu lako sasa kuhakikisha tunapata wachezaji wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi,na njia ya kufikia hili ni moja tu.Ingia kwenye timu zetu za taifa za vijana kuanzia chini ya maika 17 hadi 20, chukua vijana wenye uwezo na wenye maumbo mazuri ya soka na kuwapeleka kwenye academy za mpira za ulaya.
TFF iwape huduma kuanzia kuwalipia ada na huduma nyingine muhimu wakiwa huko. Hakika watapata nafasi ya kuonekana na watapata timu za kucheza nje ya nchi kwa maana naelewa dhahiri kuwa vipaji vipo vingi sana ila vinahitaji muendelezo tu ili viweze kuwa na faida kwa nchi.
Msiwaache wakarubuniwa na vilabu tajiri Tanzania maana ndio utakuwa mwisho wa kisoka. Hivi vilabu vina pesa na ushawishi mkubwa ambao kwa maisha ya kitanzania ni kama ndoto kushika hizo pesa. Wapelekeni nje ya nchi kwenye academy kubwa na hapo watakuwa wapo njia ya panda ya kwenda kucheza ligi kubwa Ulaya.
Najua ni gharama kutekeleza hili ila naamani kuhudumia watoto 10 ulaya kwa mwaka haiwezi kufikia hata robo ya gharama za kuiandaa timu ya taifa ambayo inakaa kambini siku kibao tu.
Mh Raisi nadhani nimejaribu kufikisha maoni yangu kwako kwa njia hii. Tanzania yenye mafanikio inawezekana. Tatizo letu sio Jezi, sio jina la timu wala sio kocha. Hata akiletwa Ferguson au Joachim Low bado timu yetu ya taifa itakuwa na matokeo mabovu.
“MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU IBARIKI AFRIKA”
0 comments:
Post a Comment