Searching...
Image and video hosting by TinyPic
26 August 2014
Tuesday, August 26, 2014

Ujio wa Madrid na maisha ya Mlinzi wa Ikulu.


Na Chicoti (Cico cicod)
 0755 700 076


Mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania X1 dhidi ya Real Madrid Legends ilipigwa kwenye uwanja wa Taifa, timu ya Real Madrid kutoka Hispania iliyokuwa na wachezaji wakongwe wa timu hiyo ilishinda kwa magoli matatu kwa moja. 

Ni mechi iliyovuta hisia za wapenzi wa soka nchini hasa ikizingatiwa Real Madrid ilihusisha wachezaji kama Luis Figo, Christian Karembeu na Fabio Cannavaro ambao kwa vipindi tofauti waliichezea Madrid. 

Ni mechi ambayo iliwapa burudani stahiki wapenda soka walioweza kufika uwanja wa taifa na ambao walibahatika waliweza kupata sahihi (autograph) za Figo ama Karembeu na wachezaji wengine wa Real Madrid ambao kwa wengi ilikuwa ndoto kuwaona “live” achilia mbali kupata sahihi zao. 

Pamoja na kupata burudani hiyo adimu kwa mashabiki wa soka bado najiuliza ujio wa Real Madrid umekuwa na faida gani kwa soka la Tanzania, sikatai inawezekana kuna faida kwenye sekta ya Utalii hasa ikizingatiwa watapata wasaa wa kutembelea vivutio vya utalii ila 

Real Madrid ni klabu ya soka tena klabu kubwa duniani hivyo nilitegemea kuona viongozi wa vilabu vya soka nchini na hasa TFF kuangalia uwezekano wa kuwa na mahusiano ya kisoka dhidi ya Madrid swala ambalo labda lingezaa vijana wa kitanzania kupelekewa kwenye “academy” za pale Hispania na kwingineko duniani. 

Sikatai timu kama Real Madrid kuweza kufika nchini si kitu kidogo iwe kwasababu za kimpira ama kitalii hasa ukizingatia mchezaji kama Figo hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Afrika ila bado tungeweza kuangalia uwezekano wa wachezaji hawa kuwa na “foundation” za soka hapa nchini ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kutengeneza mazingira mazuri kwa soka la vijana kukua. 

Lakini sitashangaa kina Figo, Karembeu na Cannavaro wakirejea katika nchi zao wakiikumbuka Tanzania kwa mavuvuzela ya uwanja wa taifa na mashuka ya kimasai kama zawadi lakini tukakosa fursa ya kuwafanya wao kama mabalozi wa soka letu kwenye nchi zao. 

Mwezi Juni mwaka 2010 timu ya taifa ya Brazili maarufu kama “selecao” walikuja nchini Tanzania kucheza mechi ya kirafiki dhidi ta Taifa Stars, mashabiki waliweza kuburudika na soka la kibrazili lakini hakuna ambacho soka letu lilifaidika sana kwa kuja kwa timu ya Brazili, ilikuwa ni fursa ya kutengeneza mahusiano ya soka na chama cha soka cha Brazili CBF lakini hilo halikutokea. 

Kama yalivyo maisha ya mlinzi wa Ikulu ambaye kila mara hupokea wageni toka nchi mbalimbali, iwe ni Maraisi, Wafalme, ama Mawaziri wakuu huku kazi yake kubwa ikiwa ni kuhakikisha usalama wa viongozi hao na labda kuwaonyesha wapi wanatakiwa kupaki magari yao lakini maisha ya mlinzi huyu hayabadiliki pamoja na kukutana na watu mashuhuri kama hao zaidi maisha yake kila panapokucha ama yabaki kuwa kama yalivyo au yazidi kudidimia zaidi. 

 Baada ya miaka mingi kupita mlinzi huyu atazeeka na kitakachompa faraja ni hadithi atakazowahadithia wajukuu wake kwamba aliwahi kumfungulia geti la Ikulu George Bush, Nelson Mandela na Obama walipokuja nchini Tanzania lakini atakuwa anayasema hayo katika wakati ambao hata mlo mmoja kuupata utakuwa ni tatizo kwake. 

Maisha ya mlinzi huyu ndivyo  hivyo itakavyokuwa kwa soka letu tutabaki na hadithi tamu za kufurahisha kuhusu kupiga picha na Figo, Cannavaro, Kaka, Robinho ama hata kushikana nao mikono na kupata sahihi zao huku soka letu likizidi kudidimia bila ya kutumia fursa ya kuja kwa Real Madrid nchini. 

NAWASILISHA

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!