Na Oscar Oscar Jr
Unapozungumzia wachezaji bora wa kigeni kwenye ligi kuu Tanzania bara kwa miaka mitano ya hivi karibuni, huwezi kuacha kumtaja kijana kutoka nchini Uganda, Emmanuel Okwi bila kujali kama wewe ni shabiki wa Simba au Yanga.
Okwi ni moja ya wachezaji waliobarikiwa kipaji cha soka, amebarikiwa nyota ya kuabudiwa hapa nchini na kubwa kuliko yote, amebarikiwa kuwa mtoto wa Kariakoo.
Okwi alikuja Tanzania kuitumikia klabu ya Simba bado akiwa kijana mdogo kabisa. Anapafahamu Morogoro vizuri kuliko kule Entebbe, anapafahamu Tanga vizuri sana kuliko Jinja na pia,anapafahamu Dar es salaam sana kuliko Kampala! Utamueleza nini Okwi? Anafahamu udhaifu wa klabu zetu na anajua mahali pa kuzibania ukutani. Utamueleza nini mtoto wa Kariakoo?
Namtazama Okwi aliyetoka SC Villa na kujiunga na wekundu wa msimbazi miaka kadhaa iliyopita, namtazama Okwi aliyekwenda Tunisia kujiunga na Etoile Du Suhel, mwisho namtazama Okwi aliyejiunga na klabu ya Yanga, kisha nagundua kabisa kuwa, huyu ni "Starling" mmoja kwenye filamu tatu tofauti.
Siku hizi Okwi anatengeneza zaidi migogoro kila anako kwenda kuliko idadi ya magoli anayofunga, anauwezo mkubwa wa kuwapiga chenga mezani viongozi kwenye majadiliano ya mkataba wake kuliko anavyoweza kuwatoka mabeki wa timu pinzani uwanjani. Huyu ndiyo Okwi mtoto wa Kariakoo.
Okwi amefanikiwa kuichezea Yanga michezo sita kwenye mzunguko wa pili wa ligi na michuano ya klabu bingwa Afrika. Amefunga mabao matatu tu lakini Kwa sababu ya kumuangalia kwa jicho la huba, jicho la mahaba, kuna watu bado wanampa sifa nyingi kuliko Mrisho Ngassa aliyefunga mabao 13 ya ligi. Tumerogwa
?
Okwi bado anauwezo wa kumpiga chenga beki wa kwanza na wa pili, lakini hana uwezo wa kumtoka beki wa tatu na kufunga bao. Okwi amepungua uwezo, sio yule tena. Anahitaji muda na nidhamu ili kuweza kurejea kwenye makali yake.
Alipoteza muda mwingi sana kwenye soka la ushindani baada ya kuingia kwenye mgogoro na klabu ya Etoile Du Suhel na hata alipotua kuitumikia The Cranes kwenye michuano ya CECAFA mwaka jana, hakuwa Okwi yule ninayemfahamu.
Bado klabu za Tanzania zinampapatikia, bado Okwi anaabudiwa, bado wanadhani ndiyo yule aliyehusika kwenye ushindi wa bao 5-0 kwenye mechi ya Simba na Yanga. Tumerogwa?
Ni rahisi sana kwa Okwi kurudi tena kuitumikia klabu ya Simba, ni rahisi sana kwake kujiunga na timu ya Azamu au timu yoyote ile kwenye ligi kuu Tanzania bara lakini, hawezi kurudi tena Etoile Du Sahil. Unajua sababu? nirahisi tu. sisi tunafumbua macho lakini hatuoni kama wanavyofanya wenzetu!
I'm sorry!
0 comments:
Post a Comment