Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 August 2014
Wednesday, August 06, 2014

SHABAAN KISIGA “MARLONE “ SIO MCHEZAJI BALI NI MWALIMU PALE MSIMBAZI


 Na Mwandishi wetu

Jioni moja sitakuja kuisahau maishani mwangu katika michezo wa soka, maana nilibahatika kumuona mmoja kati ya mafundi wa soka Tanzania kwa zama zangu.

Achana na hao wa zamani ambao walicheza soka wakati sijazaliwa. Nilikuwa naingia zangu uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa upande lango kuu la uwanja huo.Wakati nipo getini hata sijakaa vizuri nikashtukizwa na Goli la Ajabu linalogonga mwamba na kuingi Nyavuni.

Ulikuwa ni mchezo wa kirafiki baina ya Polisi Moro na Moro United Katika maandalizi ya ligi kuu mwaka 2003. Namuona mchezaji akiwa amevalia jezi number 13 mgongoni kama sikosei, sikumjua kwa jina maana alikuwa mchezaji mgeni katika kikosi cha timu ya Moro United ambacho kilisumbua sana miaka hiyo. 

Wakati naendelea kupata burudani nikashangaa kuona wachezaji wawili wakipigwa kanzu na kijana huyo huyo mwenye jezi namba 13 mgongoni, wapenda soka wanashangalia kama kawaida yao. Hapo ndipo napata akili kumtilia maanani mchezaji huyo mpya katika kikosi hicho. 

Ana umbo dogo, hana nguvu sana ila ana stamina ya kutosha. Anajua kupiga chenga, anajua kupiga mashuti na zaidi ya yote ni fundi wa kupiga pasi za mwisho. 

Na siku hiyo ndiyo siku ya kwanza kumjua fundi wa mpira Shabaan Kisiga “Marlone”. Toka kipindi hicho hadi sasa ni takribani miaka 11 lakini sikuwahi kumuona akibadilika, Ufundi wake upo pale pale na zaidi ya yote anazidi kuwa na nguvu japokuwa umri wake kwa sasa unamtupa mkono kwa kasi. 

Sikuwahi kumshangaa shabiki wa Prison aliyefunga safari kutoka Mbeya hadi Moro kuja kumuangalia fundi huyu katika pambano la watani wa jadi Simba na Yanga kwenye fainali ya Ligi ndogo Tanzania bara mwaka 2007.

Katika maisha yangu ya soka nilifanikiwa kumuona yeye na Kiungo wa zamani wa Coastal Union, Moro United na Yanga Waziri Mahadhi “Mendieta”. 

Na ndio maana pambano hilo la fainali mwaka 2007 lilikuwa na ufundi wa aina yake kwa sababu kati kati ya Dimba kulikuwa na mpambano wa kuonyesha ufundi kati ya Mendieta na Marlone. 

Muongo mmoja sasa umepita, lakini viongozi wenye busara wa simba wakaona umuhimu wa kuendelea kupata huduma hii muhimu ya Marlone.

Unadhani simba wamekosea? Hapana wapo sahihi sana. Kwa jinsi  simba walivyokuwa wanasaka kiungo mzoefu,
Mzalendo na fundi wa kuwachezesha wakina Amis Tambwe na Elias Maguli.

Walikuwa wana option mbili, nazo ni kurudisha moja ya viungo wao wa zamani kati ya Haruna Moshi “Boban” na Shaban Kisiga “Marlone” au kuwarudisha wote kwa pamoja. Tangu zama za hawa viungo zipite bado sijaona mchezeshaji mwingne wa Tanzania.

Wapo vijana wanajaribu lakini wengi wao wanatumia nguvu nyingi kuliko akili, na zaidi wengi wao wanajua kupiga pasi tu lakini si pasi zenye madhara.

Nafasi ya kiungo mchezeshaji haihitaji nguvu sana, inahitaji ufundi wa hali ya juu na akili binafsi ya kubadilisha mchezo pale timu yako inapokuwa imezidiwa. NAAM!!!!!!! hapa ndio nasema Simba wamefanya maamuzi sahihi. 

Karibu sana Marlone Msimbazi, naamini uwepo wako utakuwa ni darasa tosha kwa chipukizi Said Ndemla, Ramadhani singano,William Lucian, Haruna Chanongo na Jonas Mkude.

Hawatajifunza tu kucheza mpira na ufundi wako bali watajifunza ni namna gani wanaweza kulinda na kutunza vipaji vyao wakadumu katika soka la ushindani kwa muda mrefu na hatimae kuwa lulu ya Taifa letu kwa baadae. 

Wenzetu ulaya wamefanikiwa katika kutunza vipaji vyao, na klabu zimefanikiwa kuwatunza wachezaji wenye umri mkubwa ili kuwa “icon”ya timu kwa baadae. 

Najua wapo vijana pale Msimbazi watamdharau fundi huyu kwa kuwa wao wamesajiliwa kwa pesa nyingi kuliko Kisiga, au kwa kuwa wao wapo Timu ya Taifa wakipata Posho na ulaji wa kila namna.

Ila nawaasa wajifunze zaidi kupitia yeye. Kwa soka la Tanzania kucheza miaka 10 na zaidi kwa kiwango cha hali ya juu ni kitu cha kujifunza sana haswa kwa hichi kizazi cha sasa kinachochipukia. Namalizi kwa kusema.

UWEPO WA MARLONE MSIMBAZI UNA UMUHIMU MKUBWA KULIKO INAVYODHANIWA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!