WENGER AMEANZA KUPOTEZA MATUMAINI.
Na Oscar Oscar Jr
+255789784858
Arsene Wenger ametoa changamoto kwa wachezaji wa Arsenal watumie mechi ya nusufainali ya Kombe la FA Jumamosi dhidi ya mabingwa watetezi Wigan kujipa motisha.
Timu hiyo ya Wenger itaelekea Wembley ikiwa roho chini baada ya mfululizo wa matokeo mabaya kuzima matumaini yao ya kushinda Ligi ya Premia na kuwaacha wakipigania nafasi ya kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Kichapo kikali cha 3-0 wikendi iliyopita wakiwa na Everton kilikuwa pigo kuu kwa matumaini ya Gunners kumaliza katika nne bora na motisha katika klabu hiyo iko chini baada ya kushindwa mechi nyingi kuu msimu huu.
Arsenal walikuwa tayari wametandikwa na Manchester City, Liverpool na Chelsea, lakini kushindwa kwao na Everton ndiko kunakoweza kuwagharimu zaidi kwani Toffees hao watawapita na kukalia nambari nne kama watashinda dhidi ya Sunderland siku ya Jumamosi.
Katika hali hii, Wenger anajua kwamba Arsenal wanahitaji kupata motisha wa kukaribia kushinda taji lao la kwanza tangu waliposhinda Kombe la FA mara ya mwisho 2005.
"Lililo muhimu zaidi baada ya uchezaji wetu dhidi ya Everton ni kujibu vyema. Hapo ndipo maisha yetu ya siku za usoni yapo, uwezo wetu wa kujibu kwa uchezaji stadi na hilo lafaa kuwa katika mechi ijayo na mechi hiyo ni ya Kombe la FA,” Wenger alisema.
“Tumepoteza imani kiasi, ungeona hayo dhidi ya Everton kwa sababu mambo yote yalituendea mrama.”
Kiungo wa kati Mhispania anayechezea Arsenal Santi Cazorla aliongezea hisia kwamba msimu uko hatarini kutibuka aliponukuliwa wiki hii akisema kwamba anaweza kuhama kwa sababu wachezaji wenzake “hawana msukumo wa kushinda”.
Na hata Wenger, ambaye huwa jasiri sana anapoulizwa kuhusu udhaifu wa timu yake, alihangaika kuelezea matumaini yao huku akikabiliwa na mwisho mbaya wa msimu.
“Wakati matokeo hayaendi vyema, unaweza kila mara kufikiria kwamba unaweza kujiimarisha,” akasema.
"Hakuna timu iliyo sawa kabisa na tutajaribu kuboresha kikosi chetu na timu yetu.
Msimu huu tuliwapoteza wachezaji muhimu vipindi muhimu vya msimu, lakini lazima sasa tuangazie kumaliza vyema msimu kadiri ya uwezo wetu.”
Kuongezea masaibu ya Wenger, ni orodha ndefu ya majeraha ya viungo wa kati ambayo yanaifanya vigumu kwa timu hiyo kujikwamua.
Mesut Ozil na Jack Wilshere bado hawajarudi, huku Mathieu Flamini akiwa amesimamishwa kucheza, Alex Oxlade-Chamberlain na Tomas Rosicky nao bado wanang’ang’ana kuwa sawa kucheza.
Aaron Ramsey anapangiwa kuanza mechi kwa mara ya kwanza tangu Desemba baada ya kupona jeraha la paja.
"Tuna mengi yasiyotabirika,"Wenger alisema. “Kwa sasa tuna wachezaji wengi sana walio nje na ni muhimu warudi.”
0 comments:
Post a Comment