|
|
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ameshinikiza viungo wake waonyeshe jibu mwafaka nyumbani dhidi ya Swansea Jumanne ya leo baada ya janga la kichapo cha 6-0 mikononi mwa Chelsea wikendi iliyopita katika ligi ya Premier ya Uingereza.
Viongozi hao wa ligi hiyo waligeuza siku ya kuazimisha mechi 1000 chini ya utawala wa Wenger kuwa majonzi kwa Arsenal ambao walisambaratika kwa mara nyingine dhidi ya washindani wao wakuu katika harakati za kunyakua taji la Premier baada ya kuadhibiwa 5-1 na Liverpool na 6-3 na Manchester City mapema msimu huu.
“Ligi ya Premier ni ngumu na punde tu unapoangusha kiwango chako kidogo, utatumbukia hatarini. Hilo hutokea kwenye vilabu vingi kwasababu vita dhidi ya kushuka daraja ni kali mno,” Wenger aliwaambia watangazaji wa klabu hicho baada ya kufutilia mbali kongamano la wanahabari Jumatatu.
“Mapambano katika kilele cha ligi pia ni makali kwa hivyo kila mechi ina ugumu wake unaostahili kumudu,” aliongeza.
Arsenal walijikuta nyuma kwa bao 3-0 ndani ya dakika 17 za mechi wao kuanza ugenini Stamford Bridge huku wakiwa wamepunguzwa hadi wachezaji 10 pale Kieran Gibbs alipoonyeshwa kadi nyekundu kwa makosa baada ya mwenzake Alex Oxlade-Chamberlin kufanya masiara kwenye eneo la hatari.
Arsenal wanatumaini kosa hilo limerekebishwa na wachezaji wake watakuwa huru kuivaa timu ya Swansea katika kivumbi cha Jumanne ya leo.
“Tuna maarifa ya kutosha na tunajali maslahi ya klabu hii, bila shaka, tulisikitishwa na onyesho letu. Naamini kuwa Man City ilikuwa tofauti lakini dhidi ya Liverpool na majuzi, tulipatikana mara mbili katika mwanzo wa mechi zilizoandaliwa mapema (majira ya 12:45 alasiri),” Wenger aliendelea.
Arsenal wamo nafasi ya nne, alama saba nyuma ya Chelsea ingawa wana mechi moja ya ziada.
0 comments:
Post a Comment