Na Boniface Wambura
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza imeondoka leo (Machi 26 mwaka huu) kwenda Brazil kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani. John Kadutu ambaye ni mjumbe wa Bodi ya kituo hicho, na pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mwanza ndiye kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya Tanzania. Michuano hiyo ya siku 10 inayoshirikisha watoto wa mitaa (wavulana na wasichana) inaanza keshokutwa (Machi 28 mwaka huu). Nchi 19 zinashiriki michuano hiyo itakayofanyika katika Jiji la Rio de Janeiro.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kwa upande wa wavulana ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.
Mwaka 2010 mashindano hayo yalifanyika Durban, Afrika Kusini ambapo pia Tanzania ilishiriki.
MABINGWA WA MIKOA WATAKIWA MACHI 30
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linavikumbusha vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwa vinatakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu. Majina ya mabingwa yanatakiwa kuwasilishwa pamoja na usajili wa wachezaji waliotumika kwenye ligi ya mkoa.
Kila klabu inaruhusiwa kuongeza wachezaji watano kutoka ndani ya mkoa husika, ambapo unatakiwa uthibitisho wa usajili huo. Mpaka sasa ni vyama viwili tu ndivyo vimeshawasilisha mabingwa wao. Vyama hivyo ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo bingwa wake ni Kiluvya United, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi (LIREFA) ambapo bingwa ni Kariakoo SC.
KAMATI YA SHERIA KUPITIA MAREKEBISHO YA KATIBA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana mwishoni mwa wiki kupitia taarifa ya utekelezaji wa agizo la wanachama kurekebisha katiba zao.
TFF tulitoa agizo kwa wanachama wetu kufanyia marekebisho katiba ikiwemo kuingiza Kamati ya Maadili. Mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo ulikuwa Machi 20 mwaka huu. Hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapokea taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Sekretarieti, na baadaye kutoa mwongozo wa hatua inayofuata.
Boniface Wambura Mgoyo Media and Communications Officer Tanzania Football Federation (TFF)
25 March 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment