AZAM, YANGA VIWANJANI DAR, TANGA VPL
Na Boniface Wambura
Timu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara zinashuka tena
viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania pointi tatu. Azam yenye
pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Mgambo Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL
ikiwa na pointi 19. Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa
mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga
ipo nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47. Hata
hivyo, timu hiyo ina mchezo mmoja mkononi.
Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina
pointi 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi
hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la
Kwanza (FDL).
Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya
Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na
mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine),
Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na
Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa
Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na
Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.
Tayari tumeanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa Machi 22 mwaka huu mjini Tabora tumezuia sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000. Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba.
Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106. Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu, vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine. Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande mmoja unataka kufanya hivyo.
25 March 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment