Meneja wa Manchester
United David Moyes anaamini kwamba Juan Mata aliyenunuliwa pesa nyingi
anaweza kuziba pengo la Robin van Persie wakati wa debi dhidi ya
Manchester City uwanjani Old Trafford Jumanne.
Van Persie ambaye ni straika wa Uholanzi anatarajiwa kuwa nje ya
uchezaji wiki sita hadi nane kutokana na jeraha la goti ambalo huenda
likaacha kiungo wa kati wa Uhispania Mata, ambaye alijiunga nao kutoka
Chelsea kwa £37.1 milioni Januari, akicheza
kati.
Tangu kutua kwa Mata, amekuwa akichezezwa winga ya kulia kuwezesha Moyes kutumia Van Persie na Wayne Rooney.
Moyes amefurahishwa na uchezaji wa Mata, hasa wakati wa ushindi wa
2-0 wakiwa West Ham Jumamosi na anatarajia afae zaidi wiki chache zijazo
huku mabingwa hao wa Ligi ya Premia ambao wamehangaika msimu huu,
wakiwa alama 11 kutoka nambari nne kwa sasa, wakijaribu kukwamisha
juhudi za City za kushinda taji msimu huu.
City kwa sasa wako namabri
tatu.
"Hakuna klabu yoyote Ulaya au duniani ambayo haingependa kuwa na
Robin van Persie akicheza kama fowadi wa kati na kwetu hilo ni pigo
kubwa,” Moyes alikiambia kikao cha wanahabari Jumatatu.
"Alibadilisha mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (kwa kufunga mabao
matatu wakati wa ushindi woa wa 3-0 mechi ya marudiano Old Trafford
kabla ya kujeruhiwa huku United wakipata ushindi wa jumla wa 3-2 kwenye
16 bora dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki) kwa mabao aliyofunga lakini
lazima niseme kwamba Juan Mata alikuja hapa kucheza nafasi mbili au
tatu tofauti.
“Ninafikiri Juan aliingia na kucheza vyema Jumamosi, Amecheza vyema
katika mechi zote lakini Jumamosi alikaribia sana kufunga na labda
angefunga mara kadha,” akaongeza Moyes kuhusu ushindi ambao Rooney
aliwafungia mabao mawili.
United walilazimika kutumia Michael Carrick beki ya kati wikendi
kutokana na kutokuwepo kwa Jonny Evans, Chris Smalling, Nemanja Vidic na
Rio Ferdinand.
Moyes hakueleza ikiwa mmoja wao atakuwepo mechi hiyo dhidi ya City
ingawa Ferdinand anaweza kurejea baada ya kuuguza maumivu ya mgongo.
Mdosi huyo kutoka Scotland, ambaye yuko msimu wake wa kwanza United
baada ya kurithi mwenzake Alex Ferguson, meneja aliyefanikiwa zaidi kwenye soka la Uingereza, alisema hana wasiwasi kuhusu kumtumia Carrick katika
nafasi hiyo tena na kwamba pia atatafakari uwezekano wa kutumia beki wa
kushoto Patrice Evra, ambaye alipumzishwa wikendi, sehemu ya kati.
"(Carrick) alifanya vyema kati na sina shida. Alikuwa amewahi kucheza
hapo awali hivyo halikuwa tatizo. Hata tulikuwa tumetafakari kuweka
(Marouane) Fellaini hapo tena, kwa hivyo tuna watu wa kutosha tukihitaji
kufanya hivyo.
“Tulimpumzisha Pat Evra na tukitaka, tunaweza kumuweka hapo na anaweza kufanya vyema. Ilikuwa vyema kwamba kikosi kiliweza.”
Ushindi wa 1-0 dhidi ya Arsenal uwanjani Old Trafford Novemba ndio
wakati pekee ambapo United wameilaza timu ambayo ni moja ya tisa
zinazoongoza kwenye Ligi ya Premia msimu huu.
0 comments:
Post a Comment