SPURS WANAENDELEA KUWAFUKUZIA ARSENAL
Gylfi Sigurdsson alifunga bao la ushindi dakika ya mwisho baada ya Christian Eriksen kufunga mawili na kusaidia Tottenham Hotspur kujikwamua kutoka 2-0 chini na kuilaza Southampton 3-2 katika Ligi ya Premia Jumapili.
Sigurdsson alifunga bao kutokana na kiki ya raia wa Denmark Eriksen na kuweka hai matumaini ya Spurs ya kumaliza katika nne bora. Wamo nambari tano na alama 56, sita nyuma ya Arsenal walio wa nne wakiwa wamecheza mechi moja zaidi.
“Lazima utafute njia ya kushinda, haukuwa mteremko, haukuwa uchezaji wa kupendeza lakini mwishowe lazima utafute njia ya kushinda,” meneja wa Spurs Tim Sherwood aliambia wanahabari.
“Tumejikwamua na baada ya mechi mbili au tatu za vichapo, tumeonyesha ustadi wetu na hilo ndilo natafuta.”
Southampton walitawala mechi mwanzoni wakiwa na soka safi ya nipe nikupe na makosa mawili kutoka kwa beki wa kulia wa Spurs Kyle Naughton yaliwezesha wageni hao kuwa mbele 2-0 baada ya dakika 28.
Jay Rodriguez aliutupia mpira eneo la hatari baada ya Naughton kukosa kuupata vyema mpira uliokuwa umeondolewa na kipa Artur Boruc, na kuwezesha Rodriguez kupata fursa ya kuteka macho ya meneja wa Uingereza Roy Hodgson.
Rodriguez, mmoja wa wachezaji wa Saints anayesaka nafasi katika kikosi cha Kombe la Dunia cha Hodgson alimbwaga kipa wa Spurs Hugo Lloris na kufunga bao lake la 15 msimu huu baada ya dakika 19.
Saints waliongeza la pili baada ya Naughton kufanya kosa tena na kukosa kuondoa mpira vyema jambo lililomuwezesha Adam Lallana mwishowe kumbwaga Lloris na kufunga la pili.
Kosa jingine, wakati huu kutoka kwa beki wa kulia Nathaniel Clyne, liliwezesha Spurs kurejea tena kwenye mechi dakika nne baadaye aliporuhusu krosi kutoka kwa Naughton ipite chini ya miguu yake na kufikia Eriksen aliyefunga kutoka karibu sana na goli.
Dakika moja baada ya kipindi cha pili kuanza, Spurs walisawazisha baada ya Roberto Soldado kumzidi nguvu difenda Dejan Lovren na kutoa krosi kwa Eriksen ambaye alifunga tena.
Sigurdsson, aliyeingia kama nguvu mpya baada ya mapumziko kuchukua nafasi ya Moussa Dembele, alikamilisha ushindi kwa kombora la chini dakika za mwisho.
0 comments:
Post a Comment