Searching...
Image and video hosting by TinyPic
23 March 2014
Sunday, March 23, 2014

MESSI SHUJAA WA EL-CLASSICO


Mabingwa wa ligi ya Uhispania, La Liga, Barcelona walisonga hadi alama moja nyuma ya vingozi wa sasa pale walipowachakaza maasimu wao wa jadi, Real Madrid, 4-3 katika kivumbi cha kusisimua cha El Clasico Jumapili. 

Mshambuliaji wa Argentina, Lionel Messi, aliibuka nyota katika mechi hii ambayo ilisubiriwa kwa hamu duniani kote kwa kufunga magoli matatu katika uwanja uliojaa pomoni wa Bernabeu huku akiandikisha rekodi ya mabao zaidi katika El Clasico pale alipofikia 19. 

Katika mechi iliyojaa bwembwe za aina yake na soka la kuwacha vinywa wazi, Andreas Iniesta aliwapa wageni uongozi katika dakika ya saba kwa kombora safi lililomwacha Diego Lopez katika lango la Madrid bila jibu pale alipopokea pasi safi kutoka Messi. 

Messi na mwenzake nyota wa Brazil, Neymar, walikosa nafasi muruwa za kufanya mambo 2-0 kwa faida ya Barcelona waliohitaji kushinda mechi hii ili kudumisha matumaini ya kuhifadhi taji lao katika mwanzo wa kasi sana katika mechi hii. 

Baada ya kuduwazwa, Madrid waliinuka pale kiungo Angel Di Maria, alipochukua utawala na kuleta krosi iliyotiwa kimyani kwa kichwa na straika wa Ufaransa, Karim Benzema katika dakika ya 20 na wawili hao waliungana tena kuwapa wenyeji uongozi wa 2-1.

Di Maria kwa mara nyingine alitimuka kutoka kushoto na baada ya mlinda ngome Javier Mascherano kukosa mwelekeo na kushindwa kumudu krosi yake, Benzema alimfunga kipa Victor Valdes ambaye hakuwa na linguine ila kusalimu amri. 

Beki Gerard Pique, aliokoa Barcelona dakika chache baadaye na kutibua juhudi za Benzema kupata lake la tatu baada ya kuunganishiwa tena na Di Maria ambaye alikuwa mwiba katika ngome ya wageni. 

Mabingwa hao ambao wamemudu shutuma kali kuhusu uwezo wao kutamba hawakukata tama na dakika mbili kabla ya mapumziko, Messi alisawazisha baada ya kudhibiti mpira ndani ya eneo la hatari na kumuelemea Lopez. 

Benzema alikosa fursa nyingine ya wazi baada ya mpira wake wa kichwa kutoka krosi ya Dani Carvajal ulipokosa lango kwa inchi chache. 

Kipindi cha lala salama kilianza na Benzema alipomshinikiza Valdes kuokoa kombora la ana kwa ana baada ya kupokea pasi kutoka Gareth Bale, aliyetimuka kati ya ngome ya Barcelona kwa hima kuu. 

Madrid hatimaye walichukua uongozi dakika 55 pale walipopewa penalti ya utata pale nyota wao, Cristiano Ronaldo, alipotegwa na Dani Alves, ingawa picha za runinga zilionyesha kuwa kosa hilo lilifanyika nje ya eneo la hatari. 

Ronaldo aliinuka na kupachika boli wavuni chini ya mkono wa kulia wa Valdes aliyesoma nia yake kwa ustadi lakini hakufanikiwa kuokoa bao. 

Huku Real wakiendelea kudhibiti maadui wao, taswira ya mechi hii ilibadilika pakubwa ikisalia dakika 25 pale Messi alipomwachilia Neymar na pasi ya unyoya na mbio za straika huyo wa Brazil zilisitishwa na Sergio Ramos katika eneo la hatari. 

Refa hakuwa na linguine ila kuashiria penalti na kuwaongezea Real masaibu pale alipomlisha kadi nyekundu kapteni wao na Messi alichukua jukumu na kufanya mambo kuwa 3-3. 

Alves aligonga ulingo wa lango kutoka hatua 25 huku Barca wakiongeza mashambulizi na walipata uongozi pale walipopata penalti ya pili baada ya Iniesta kuangushwa kwenye eneo nyeti.
Matokeo yalikuwa yale, yale, pale Messi alipotinga bao lake la tatu kutoka hatua 12, wakati huu, akipachika mpira juu ya lango la Lopez. 

Ililkuwa mara ya kwanza katika mechi 32 kwa Real kuonja kichapo na inamaanisha Atletico Madrid, waliwabwaga Real Betis 2-0 hapo awali Jumapili, wanabakia viongozi wa La Liga.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!