Searching...
Image and video hosting by TinyPic
26 March 2014
Wednesday, March 26, 2014

MAMBO SI SHWARI KWA DAVID MOYES



Edin Dzeko alifungia Manchester City mabao mawili na kuiongezea masaibu Manchester United kwa kuwapokeza kichapo cha 3-0 Jumanne uwanjani Old Trafford. 

Ushindi huo umepunguza mwanya kati ya City na viongozi wa Ligi ya Premia Chelsea hadi alama tatu wakiwa na mechi mbili ambazo hawajacheza. 

Dzeko alichukua sekunde 43 pekee baada ya mechi kuanza kuwapa City uongozi kwenye debi hiyo ya Manchester.
Rafael alimzima David Silva aliyekuwa akikimbia eneo la hatari lakini Samir Nasri akagonga mlingoti kwa kombora lake kabla ya Dzeko kupata mpira uliodunda na kuutuma wavuni. 

Straika huyo wa Bosnia alifunga tena dakika ya 56 pale alipomuelemea Rio Ferdinand na kufunga kona ya Nasri. Yaya Toure naye alitonesha kidonda cha United kwa bao la tatu dakika ya 90 huku vijana hao wa Manuel Pellegrini, ambao sasa wako nambari mbili kwenye msimamo wa ligi, wakishinda debi yao ya pili sasa baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya United Eastlands Septemba mwaka. 

Ulikuwa ni usiku mwingine ambao mdosi wa United David Moyes atataka sana kusahau, msimu wake wa kwanza akiwa kiongozi wa mabingwa hao wa ligi Uingereza baada ya kustaafu kwa Alex Ferguson, meneja aliyefanikiwa zaidi katika soka ya Uingereza. 

Matokeo hayo yaliacha United wakiwa alama 12 nyuma ya timu nne bora na sasa watalazimika kushinda Ligi ya Klabu Bingwa msimu huu, ndipo wafuzu kwa dimba hilo kuu Ulaya msimu ujao. 

Arsenal, ambao walikuwa tu wametoka kula kichapo cha aibu cha 6-0 mikononi mwa Chelsea wakati wa mechi ya 1 000 ya Arsene Wenger akiwa kashika usukani wikendi iliyopita, walilazimishiwa sare ya 2-2 na Swansea ambayo imekuwa ikihangaika msimu huu, kwenye mechi iliyochezewa uwanjani Emirates.

Wilfried Bony alifunga krosi ya Neil Taylor na kuwapa Swansea uongozi dakika ya 11pale London.
Lakini mabao mawili dakika mbili katikati ya kipindi cha pili yalibadilisha mambo. 

Kieran Gibbs, aliyeruhusiwa kucheza baada ya kufukuzwa uwanjani kimakosa badala ya Alex Oxlade-Chamberlain dhidi ya Chelsea, alitoa krosi ambayo Lukas Podolski alifunga na kusawazishia Arsenal dakika ya 73. 

Na baada ya uchezaji kuanza, Podolski alifaa kwa kusambaza mpira, na krosi yake ilifungwa na Olivier Giroud jambo lililofurahisha sana mashabiki wa Arsenal. 

Lakini mambo yalibadilika, pale dakika ya mwisho ya muda wa kawaida, kombora la Leon Britton lilipojipinda baada ya kumgonga Wojciech Szczesny na kisha likamgonga Mathieu Flamini na kuingia wavuni na kuzaa bao la kuchekesha sana la kujifunga.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!