HATIMAYE DAVID MOYES APATA NAFASI YA KUPUMUA.
Wayne Rooney alifunga mabao mawili na Juan Mata akapata lake la kwanza la Manchester United pale mabingwa hao wa ligi ya Premier walipowalaza Aston Villa 4-1 nyumbani na kumpa meneja wao, David Moyes, nafasi ya kupumua baada ya shutuma kali.
Ashley Westwood alitishia kuwatumbukiza kwenye masaibu zaidi pale alipowapa wageni uongozi katika dakika ya 13 kupitia mkwaju wa adhabu lakini baada ya muda wa sintofahamu hekalu la Old Trafford, United walitawala kupitia Rooney, Mata na Javier Hernandez.
United walipata matokeo ya kuwapa moyo kabla ya kivumbi chao kikali katika robo fainali za kombe la klabu bingwa Jumanne ugenini mwa watetezi wa taji hilo, Bayern Munich, kwenye mkondo wa kwanza.
Baada ya kucharazwa 3-0 na waasimu wao na majirani Manchester City Jumanne iliyopita, United walijitosa uwanjani wakitafuta kukomboa hadhi yao lakini walijipata motoni pale Rafael da Silva alipomtega Gabriel Agbonlahor kwenye pembe ya eneo la hatari.
Westwood alipeperusha kombora la adhabu liloishia wavuni licha ya kipa wa United, David de Gea, kunyoosha mkono wake na kuusaka mpira bila mafanikio.
Ilichukua dakika saba pekee United kusawazisha pale Rooney alipopachika wavuni kwa kichwa kutokana na krosi yake Shinji Kagawa ambaye alitimka na mpira hadi eneo la hatari kabla ya kumuunganishia mwenzake kwa ustadi.
United walitwaa uongozi sekunde chache kabla ya muda wa mapumziko pale Mata na Rooney waliposhirikiana kuipatia United la bao la pili.
Kagawa alimlisha pasi Mata ambaye alikuwa akijiandaa kufyatua mzinga lakini Leandro Bacuna kwenye ngome ya Villa alimzuia kwa kumfyeka chini na refa Martin Artkinson hakusita kuwapatia penalti Man United iliyotiwa wavuni na Rooney.
Straika Christian Benteke alikosa nafasi mbili za wazi za kufanya mambo kuwa 2-2 mwanzoni mwa kipindi cha pili na walijuta katika dakika ya 57 pale Mata alipopata la tatu na lake la kwanza tangu kusaini kutoka Chelsea Januari.
Adnan Januzaj na Chicharito waliinuka kutoka benchi kuchangia la nne, Januzaj akileta krosi iliyo pachikwa wavuni na mshambuliaji huyo wa Mexico.
0 comments:
Post a Comment