ARSENAL WASAMBARATISHWA NA MOURINHO DARAJANI.
Mechi ya 1000 ya kocha wa Arsenal, Arsene Wenger iligeuka majonzi na kufuta sherehe za kutimiza hatua hiyo baada ya timu yake kupokea kipigo cha 6-0 kutoka kwa Chelsea katika uwanja wa Stamford Bridge Jumamosi.
Kivumbi hicho kilichotazamiwa kuwaniwa vikali na miamba hao wa London kilegeuka kuwa zoezi kwa Chelsea waliopata mabao yao kupitia straika wa mcameroon, Samuel Eto’o, mawili kutoka Oscar, Andre Schurrle, penalti ya Eden Hazard na kiungo wa Misri, Mohammed Salah, alisherehekea goli lake la kwanza tangu kujiunga na viongozi hao wa ligi ya Premier mwezi Januari.
Kufuatia kichapo hicho cha mbwa, Chelsea walisalia kileleni na alama 69, huku Arsenal, waliobaki alama saba nyuma ya majirani wao, wakibaki kutazama matumaini ya kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza kwa mwongo mmoja yakififia.
Kwenye mechi iliyokuwa na visanga kem kem, Eto'o alianza kwa kuifungia bao nzuri Chelsea dakika ya tano kabla ya mjerumani Schurrle kupata la pili dakika mbili baadaye kwa mkwaju mrefu uliomshinda kipa wa Arsenal, Wojceich Sczesny.
Penati ya Hazard baada ya Alex Oxlade-Chamberlain kunawa mpira langoni baada ya mkwaju wa kiungo huyo wa Ubelgiji kumuelemea Sczesny kulifanya mambo 3-0 baada ya robo saa.
Refa Andre Marriner, alishangaza wengi pale alipochanganyikiwa na baada ya kutokujua ni nani aliyefanya kosa, alimpa kadi nyekundu Kieran Gibbs ambaye hakufanya badala ya Oxlade-Chamberlain licha ya mshambuliaji huyo kumweleza yeye ndiye anayefaa adhabu.
Oscar alihitimisha kipindi cha kwanza kwa bao la nne kabla ya Salah kuingia kipindi cha pili na kufunga la kumpisha Oscar kufunga mahesabu na la sita.
Wenger ambaye alichukua usukani wa mechi yake ya 1000 katika utawala wa miaka 18 Arsenal alibaki kukata tama kwenye eneo lake la kiufundi huku ndoto hiyo mbaya ikiendelea mbele yake.
Mechi inayofuata, Arsenal watakutana na Swansea kisha wikiendi ijayo watawakaribisha Manchester City huku shauku ikitanda kama watakuwa na uwezo wa kujiinua tena kutoka pigo hilo.
Arsenal wameshindwa kutamba ugenini wakitembelea washindani wao wakuu kwenye ligi hiyo katika mechi za alasiri huku wakipokea adhabu ya 6-3 kwa City na 5-1 mikononi mwa Liverpool kabla ya janga la Jumamosi.
0 comments:
Post a Comment