Staa wa Uingereza, Wayne Rooney, alifunga bao la kipikee lilowaacha wengi kinywa wazi kabla ya kutinga la pili na kusaidia klabu yake Manchester United kuwachakaza wenyeji West Ham 2-0 katika uwanja wa Upton Park, Jumamosi.
Huku nyota aliyestaafu wa Uingereza, David Beckham, akitizama patashika hiyo miongoni mwa mashabiki, Rooney alionekana kuiga bao lake spesheli kutoka kati kati mwa kiwanja dhidi ya Wimbledon mwaka wa 1996 kwa kuachilia mkwaju kutoka kimo kirefu cha yadi 60 kutoka lango uliomfedhehesha kipa wa Adrian pale ulipopepea, kujipinda hewani na kudunda kabla ya kutua wavuni.
Goli hilo la kusisimua lilipatikana katika dakika ya nane pale Rooney alipomwandama mlinda ngome wa West Ham, James Tomkins, na kumwondoa hesabuni na baada ya mpira kuanguka, aliangalia juu na kuona Adrian akiwa ameasi lango lake kabla kuandikisha historia.
United waliimarisha mashabulizi na baada ya kukosa nafasi kadhaa kupitia Shinji Kagawa na Juan Mata huku West Ham wakijibu na mipira ya juu juu iliyolenga straika wao Andy Caroll ambaye alichapa nje baada ya kutia kichwa chake kwa mkwaju wa adhabu kabla ya kipa wa United, David de Gea, kuokoa jaribio lake la pili, pia kwa kichwa, muda mfupi baadaye.
Kapteni wa West Ham, Kevin Nolan, alidai penalti pale alipoangushwa na Darren Fletcher na baada ya refarii kukataa maombi hao, United walimwagika upande wa pili wa uwanja dakika ya 33 na kupata lao la pili katika shambulizi la mshtukizo.
Ashley Young alitimuka hadi pembeni ya kulia mwa uwanja na kutuma krosi ambayo ilimpata Mark Noble kwenye ngome ya West Ham na kwa bahati mbaya, jaribio lake la kufyeka mpira huo kutoka eneo la hatari lilitibuka pale alipofanikiwa kumpata Rooney aliyeuelekeza wavuni.
Hilo lilikuwa la 212 straika huyo kuifungia United na kumfanya ampite Jack Rowley, hadi nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wakuu wa miamba hao wa Uingereza nyuma yake Bobby Charlton (249) na Denis Law (237).
Kipindi cha pili kilikosa kufikia kiwango cha kutumbuiza kama cha kwanza huku West Ham wakitishia kupunguza uongozi wa United kutoka mikwaju ya kona ambayo haikufanikiwa kuzaa magoli.
0 comments:
Post a Comment