Wauza Juice kutoka jiji la Dar es salaam klabu ya soka ya Azam inaendelea kutamba kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata jana dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Ushindi huo, unaifanya Azam ifikishe pointi 50 baada ya kucheza mechi 22 na kubaki kileleni mwa Ligi Kuu, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na washambuliaji wake, John Bocco dakika ya 63 kwa shuti kali akimalizia pasi ya Mganda, Brian Umony aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Gaudence Mwaikimba.
Bao la pili lilifungwa na Umony dakika ya 82 kwa shuti kali ambalo lilimbabatiza kipa Salehe Tendega na kuingia nyavuni.
Nao wabingwa watetezi Yanga sc wameiadhibu vikali Prisons ya Mbeya kwa kuichapa mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hapo jana.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC iendelee kuwa na matumaini ya kutetea taji lake, kwani sasa inatimiza pointi 46 baada ya mechi 21, ikizidiwa pointi nne na Azam FC walio kileleni.
Magoli ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi dakika ya 20,Mrisho Ngassa dk 37,Hamis Kiiza dk 67,Nadir Haroub kwa mkwaju wa penati dk 76 na Kiiza alijipatia bao lake la pili la mchezo dakika ya 88.Mpaka dakika 90 zinamalizika,Yanga 5-0 Tanzania Prisons.
Wababe hawa wawili ni kama mapacha,wanakimbizana kila wanapotua uwanjani na sasa mechi kati ya Mbeya City vs Azam na Simba vs Yanga pengine zinaweza kuonyesha mwanga wa kujua ni nani atakaye ibuka bingwa mpya wa Vodacom Premier League msimu huu.
0 comments:
Post a Comment