Na Oscar Oscar Jr
Hatimaye ligi kuu Tanzania bara baada ya kusimama kwa muda, inarejea leo hii kwa mchezo mmoja kupigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba Sc watapambana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa mzunguko wa nane.
Baada ya mechi saba za awali, Simba walifanikiwa kujikusanyia alama tisa baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mara sita. Kwa upande wa Kagera Sugar, wao walifanikiwa kushinda mechi mbili, kupoteza mchezo mmoja na kutoka sare mara nne.
Tayari rekodi zinaonyesha namna ambavyo Kagera Sugar wamekuwa wakifanya vizuri dhidi ya vigogo na msimu huu, tayari wamefanikiwa kumfunga Yanga kwa bao 1-0 huku wakitoka sare ya kufungana bao 1-1 na vinara wa ligi hiyo timu ya Mtibwa Sugar.
Tayari Simba wamefanya usajili na kubadilisha kikosi chao kwenye safu ya ushambuliaji ambako wamemuongeza Danny Sserunkuma, watu kama Simoni Sserunkuma kwenye kiungo na kina Hassan Kessy wakiongezeka kwenye safu ya ulinzi ni wazi kuwa timu hiyo inaonekana kuimarika kwenye kila idara.
Bado Kagera Sugar wanauwezo wa kuitikisa safu ya Ulinzi ya Simba kutokana na kucheza mpira wa nguvu kwa dakika zote 90 huku wakionekana imara zaidi katika kujilinda ambapo mpaka sasa wameruhusu mabao manne pekee kutinga kwenye goli lao.
Endapo Simba wanaoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo wa leo, watapanda hadi kwenye nafasi ya nne na kuwashusha Coastal Union ambao wanakamata nafasi hiyo wakiwa na alama 11.
Ushindi kwa Kagera Sugar kwenye mchezo huo, unaweza kuwapeleka hadi kwenye nafasi ya pili na kuwashusha Yanga na Azam ambao wote wana alama 13 na wanatarajia kuumana siku ya Jumapili.
0 comments:
Post a Comment