LIVERPOOL WANAENDELEA KUMKIMBIZI MTU KIMYA KIMYA.
Chuma moto, Liverpool, waliendeleza harakati zao za kutwaa ubingwa wa ligi ya Premier ya Uingereza baada ya kuwazima Sunderland 2-1 kwenye mechi iliyo sakatwa uwanja wa Anfield Jumatano.
Nahodha Stephen Gerrard na straika matata, Daniel Sturridge, waliitunuku klabu yao uongozi wa 2-0 lakini bao kutoka Ki Sung-yueng zikisalia dakika 14 mechi kukamilika liliwatoa Liverpool kijasho lakini walifanikiwa kuwadhibiti wapinzani wao na kuzoa alama tatu muhimu.
Gerrard alifyatua kombora kali la adhabu katika dakika ya 39 kabla ya Sturridge kuongezea la pili dakika chache baadaye kipindi cha pili kungoa nanga na mkwaju ulio elekezwa wavuni na mlinda ngome wa Sundeland.
Ingawa bao la Sung-yeung liliwatia mashabiki wa nyumbani tumbo joto, vijana wa Brendan Rodgers waliweza kuhifadhi uongozi wao hadi tamati ya mchezo huo.
Akizungumuza na wanahabari baada ya mechi, Rodgers aliwapigia vijana wake upatu na kuongeza kuwa,watastahimili mvutano katika mechi za kufunga msimu baada ya kupanda hadi nafasi ya pili kwenye jadwali la Premier.
Liverpool sasa wamo alama moja nyuma ya viongozi Chelsea huku City wakiwafuata na alama mbili ingawa wamecheza mechi mbili pungufu.
“Tumekuwa na msimu wa kufana na bado kuna safari ndefu iliyobaki lakini ujumbe ni kuwa tuendelee kudumisha imani.
“Tulishamiri kwa kipindi kirefu na pindi msimu unavyoendelea, tutastahimili shinikizo ili kunawiri,” Rodgers alisema.
0 comments:
Post a Comment