Kiingilio
cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa
Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The
Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti
vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000
viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045
kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo
viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio
vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni
sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A
yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali
hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi
Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini
Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi
kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza
kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule
ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko
mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live
Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
Tunapenda
kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika
maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa
fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
0 comments:
Post a Comment