Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 December 2014
Saturday, December 13, 2014

Uchambuzi: Leicester City vs. Manchester City


Na Chikoti Cico

Katika kiwanja cha King Power Stadium wikendi hii kwenye ligi kuu nchini Uingereza timu ya Leicester City itaikaribisha timu ya Manchester City katika mtanange unaotarajiwa kuwa mkali huku kila timu ikitafuta ushindi.

Leicester City wanaofundishwa na kocha Nigel Pearson wana hali tete zaidi kwenye ligi ya Uingereza kwani mpaka sasa wanashika mkia wakiwa na alama 10 tu kwenye msimamo wa ligi nafasi ambayo inawafanya wawe kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kuelekea kwenye mchezo kocha Pearson atawakosa kipa Kasper Schmeichel ambaye atakuwa nje kwa karibi wiki sita, na Matt Upson ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu ingawa amerejea mazoezini ila hatacheza mchezo huo, nahodha wa timu hiyo Wes Morgan anatarajiwa kurejea kikosini baada ya kuwa nje akitumikia adhabu.

Kikosi cha kocha Nigel Pearson kinaweza kuwa hivi: Hamer; De Laet, Morgan, Upson, Konchesky; Mahrez, James, Cambiasso, King, Schlupp; Vardy

Leicester City wanaonekana kuwa na mwenendo mbovu kwenye ligi kwani rekodi zinaonyesha katika michezo 10 waliyocheza wamepata alama mbili tu.

Kwa upande wa Manchester City Vicent Kompany ambaye alikuwa majeruhi anatarajiwa kurejea kikosini baada ya kuwa nje kwa mechi mbili zilizopita huku pia kiungo David Silva akitarajiwa kuanza kwenye mchezo huo baada ya kuwa nje kwa wiki sita ila mshambuliaji wa timu hiyo Sergio ataendelea kukosekana.

Manchester City inayofundishwa na kocha Manuel Pellegrini mpaka sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na alama 33 wakiwa wamepitwa na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea kwa alama tatu tu.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha timu ya Manchester City haijapoteza kati ya michezo nane iliyocheza na Leicester katika mashindano yote huku ikiwa imeshinda michezo minne na kutoka sare michezo minne.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Kompany, Demichelis, Clichy; Navas, Fernando, Fernandinho, Nasri; Toure, Dzeko

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!