Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 December 2014
Saturday, December 13, 2014

Uchambuzi: Manchester United vs Liverpool


Na Chikoti Cico

 Ndiyo ni Manchester United dhidi ya Liverpool, moja ya mechi itakayovuta hisia za mashabiki wengi wa ligi kuu nchini Uingereza mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili. Takwimu zinaonyesha kuwa ni mchezo wa pili unaoongoza kuwa na kadi nyekundu nyingi kwenye ligi kuu nchini Uingereza kadi 15.

Manchester United wanaingia kwenye mchezo huo huku wakishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamejikusanyia alama 28 kufuatia ushindi wa magoli 2-1 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Southampton.

Kocha wa Manchester United Luis Van Gaal atawakosa Angel di Maria, Luke Shaw na Danny Blind ambao ni majeruhi kwenye mchezo huo ila kurejea kwa Rafael na Phil Jones kutakiongezea nguvu kikosi cha kocha huyo mdachi kwenye mchezo huo dhidi ya Liverpool.

Kuelekea mchezo huo mshambuliaji wa Manchester United Robin Van Persie ameonekana kuwa na takwimu nzuri za magoli dhidi ya Liverpool huku akiwa amefunga magoli sita katika mechi tisa alizocheza dhidi yao.

Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea; Jones, Evans, Rojo, Rafael; Carrick, Fellaini, Young, Mata; Rooney, Van Persie

Kwa upande wa Liverpool hakuna wachezaji wapya majeruhi huku mshambuliaji Mario Balotelli akitarajiwa kurejea kikosini baada ya kuwa nje kwa muda hivyo kocha wa timu hiyo Brendan Rodgers ataingia kwenye mchezo akihitaji kupata alama tatu muhimu dhidi ya wapinzani hao wa jadi.

Liverpool mpaka sasa wanashika nafasi ya tisa wakiwa na alama 21 kwenye msimamo wa ligi na hivyo kupitwa na United kwa alama saba huku wakipitwa na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea kwa alama 15.

Kuelekea mchezo huo nahodha wa Liverpool Steven Gerrard anaongoza kufunga magoli mengi kama mchezaji mgeni kwenye uwanja wa Old Trafford akiwa amefunga magoli matano, pia takwimu zinaonyesha kwamba Liverpool ni timu ya pili nyuma ya Chelsea kushinda mara nyingi Old Trafford ikiwa imeshinda mara tano.

Kikosi cha Liverpool kinaweza kuwa hivi: Mignolet, Johnson, Enrique, Lovren, Skrtel, Lucas, Henderson, Lallana, Gerrard, Sterling, Balotelli

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!