Na Chikoti Cico
Mshambualiaji wa Manchester United, Radamel Falcao ambaye amekuwa nje kwa karibu wiki nne baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya West Brom ambao uliisha kwa sare ya magoli 2-2 mwishoni mwa mwezi wa kumi, ataendelea kuwa nje kwa wiki mbili zaidi baada ya kuumia tena mapema wiki hii kwenye mazoezi ya timu ya United.
Falcao aliyesajiliwa kwa mkopo toka timu ya Monaco ya Ufaransa, mpaka sasa hakuna mchezo aliyomaliza dakika 90 huku akiwa na goli moja tu toka asajiliwe.
Kuumia tena kwa mshambuliaji kutafanya kocha wa Manchester United, Luis Van Gaal kumtegemea zaidi Robin Van Persie kuongoza mashambulizi ya timu hiyo hasa kwenye mchezo wa siku ya Jumamosi dhidi ya Arsenal utakaopigwa kwenye uwanja wa Emirates.
Taarifa za kuumia kwa Falcao zilitolewa na kocha wa United Luis Van Gaal wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo dhidi ya Arsenal.
Wakati huo huo, kiungo Angel Di Maria na kipa David De Gea ambao walipatwa na misukosuko ya majeraha kwenye mechi za kimataifa za kirafiki mapema wiki hii, wanatarajiwa kuwa fiti kuichezea United dhidi ya Arsenal hapo Jumamosi.
Manchester United ambao wanashika nafasi ya saba wakiwa na alama 16 kwenye msimamo wa ligi huku wakipitwa na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea kwa tofauti ya alama 13, wataendelea kuwakosa mabeki Rafael da Silva, Jonny Evans, Phil Jones, Marcos Rojo na kiungo Daley Blind huku beki wa kulia Luke Shaw akiwa nae kwenye hatihati ya kukosekana kwenye mchezo dhidi ya Arsenal.
0 comments:
Post a Comment