Searching...
Image and video hosting by TinyPic
3 November 2014
Monday, November 03, 2014

NIONAVYO MIMI; SIMBA ANAWEZA KUTWAA UBINGWA MSIMU HUU.


Na Oscar Oscar Jr

Ukitazama ligi ya Bundesliga kwa sasa, unakutana na Bayern Munich waliokusanya pointi 24 huku soka lao likivutia kila kukicha. Unapogeukia Hispania kwenye La Liga, unakutana na vitisho vya Real Madrid na ubora wa Christiano Ronaldo, unawaogopa balaa. 

Chelsea kwenye EPL na kiburi cha Jose Mourinho, kiukweli haijulikani ni lini watapoteza mechi yao ya kwanza, pengine muda ndiyo utaamua.

Kisha, nageuka kuitazama ligi kuu ya Tanzania bara na kuangalia anayetisha simuoni. Nageuka kulia simuoni, naangalia kushoto nako simuoni. Nagundua kuwa, ligi kuu Tanzania bara msimu huu haina timu inayotisha ila, kuna timu zina pointi nyingi kuliko nyingine.

Pamoja na Mtibwa Sugar kuongoza msimamo wa ligi kuu, bado ukiwatazama uwanjani wanacheza mpira wa kawaida sana. Pamoja na timu ya Coastal Union kushika nafasi ya pili, bado sioni kama wanatisha na kupitia hilo, bado naamini kuwa Simba haijafanya vibaya sana licha ya kutoka sare mara sita.

Unapokuwa na timu yenye uwezo wa kufunga goli kwenye kila mchezo, ni ishara ya kuimarika. Simba imefunga goli kwenye kila mchezo msimu huu kasoro mchezo wao mmoja, waliocheza dhidi ya timu ya Yanga. 

Azam wameshindwa kufanya hivyo, Yanga wameshindwa na hata Mbeya City, hawajaonyesha uwezo huo. Sikushangazwa na timu ya Ndanda kuifunga timu ya Azam 1-0 kwa sababu, Ndanda nao walikuwa wanafunga goli angalau moja kwenye kila mchezo isipokuwa dhidi ya Mgambo JKT walipolala kwa bao 1-0.

Ndanda kabla ya mchezo wao na Azam, walikuwa wanashika mkia na baada ya ushindi huo, wako nafasi ya 10. Mbeya City kabla ya mchezo wao na Mgambo, wanashika nafasi ya mwisho (14) lakini, wakishinda watafika kwenye nafasi ya sita. 

Mgambo wako kwenye nafasi ya 12, wakishinda dhidi ya Mbeya City, wanaweza kufika nafasi ya tano. Una anzia wapi kuikatia tamaa timu ya Simba?

Sio kweli kwamba UKAWA wanazuia ushindi wa Simba, sio kweli kwamba Simba inahujumiwa. Simba inatatizo la Uongozi kuingilia benchi la Ufundi, tatizo la majeruhi, Uteuzi wa kikosi cha kwanza na saikolojia ya wachezaji. 

Pamoja na wachezaji wa Yanga, Mbrazil Jaja na Coutinho kutofanya kile watu wengi walichotarajia lakini, huwezi kuona Uongozi wa Yanga ukiwaondoa wachezaji wao kikosini. 

Wanaweza kuwa hawapendezwi na namna kocha Maximo anavyowapa nafasi wabrazil hao lakini, mambo ya ufundi kaachiwa fundi Maximo. Simba wanapaswa kuiga hilo kutoka kwa watani zao.

Kilichomtokea kiungo mshambuliaji wa zamani wa Cheslsea, Juan Mata baada ya ujio wa kocha Jose Mourinho, ndicho kinachomkuta Amisi Tambwe chini ya utawala wa kocha Patrick Phiri. 

Mata alikuwa mchezaji bora mara mbili wa klabu lakini alikwenda bechi, na mwishowe akauzwa. Tambwe ndiye mfungaji bora ligi kuu msimu ulipita, ameanzia benchi na kifuatacho ni kuuzwa au kutemwa!

Ukihitaji Tambwe akabe, utakuwa unamuonea kwa sababu hakununuliwa kwa kazi hiyo. Hakuna hata siku moja Amri Kiemba aliwahi kupewa sifa kwa sababu anakaba vizuri, haijawahi kutokea. 

Unapowaanzisha kwa pamoja Tambwe, Okwi, Kisiga na Kiemba utanufaika nao pale tu mpira unapokuwa kwenye himaya yao. Wakipoteza, wanahitaji watu wa kuwakabia na kuupeleka mpira tena  kwao.

Patrick Phiri anatakiwa kujua namna ya kuwatumia wachezaji wa aina ya kina Kiemba ili aweze kupata kilicho bora kutoka kwao. Hata kelele anazopigiwa Mesut Ozil kuwa hakabi au anakimbia kilomita chake, hazina mashiko. 

Ozil huyu huyu anayetukanwa na mashabiki wa Arsenal, ukimpeleka klabu ya Chelsea akacheze nyuma ya Diego Costa au Manchester City akacheze nyuma ya Kun Aguero, hautomtofautisha na yule wa Real Madrid.

Msimu uliopita Azam walikuwa moto kweli kweli, msimu huu sioni makali ya aina ile. Mbeya City walikuwa wanaitetemesha nchi kila wanaposhuka dimbani lakini msimu huu sioni mwenye kasi ile na hata kikosi cha kocha Hans Van Der Pluijm cha Yanga, kilikuwa kinagawa dozi ya hatari lakini, bado sioni kikosi kinachofikia ubora wa msimu uliopita.

Bado Yanga na Azam ndiyo timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu licha ya kuchechemea lakini, ukitazama tofauti ya pointi kati yao na Simba, ni alama nne pekee. Siwezi kushangaa Simba kama atatwaa ubingwa msimu huu kwa sababu, ndani ya uwanja, hii ni timu inayoonyesha promise. 

Bado naiheshimu Mtibwa Sugar, bado naiheshimu Coastal Union lakini, wanapaswa kuongeza uwezo uwanjani ili kufikia malengo waliojiwekea. Tayari zimepigwa mechi sita, bado kuna dirisha la usaji na pia, kuna mechi 20 zilizosalia. Una anzia wapi kuikatia tamaa Simba?


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!