Searching...
Image and video hosting by TinyPic
10 November 2014
Monday, November 10, 2014

Karibu Arsene Wenger Uhuru Peak.


Na Oscar Oscar Jr

Uhuru Peak ni jirani sana na Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, Dar es Salaam. Hapa ni mahali ambapo mara nyingi napatikana siku za weekend kucheki mechi. 

Nilikuwepo maeneo hayo wakati Alexies Sanchez anafunga bao kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Leicester City, Nilikuwapo tena wakati Arsenal wanatoka sare ya 2-2 dhidi ya Hull City na jana, nilikuwepo pia wakati Arsenal anafungwa bao 2-1 na Swansea City.

Wakati Arsenal akifungwa jana na Swansea City, pembeni yangu alikuwepo shabiki wa Arsenal. Baada ya goli la Sanchez kufungwa, jamaa aliagiza vinywaji meza yote kwa shangwe. 

Wakati muhudumu akianza kufungua vinywaji, Swansea wakasawazisha goli. Wakati tunaanza kunywa, Swansea wakapiga goli la pili. Unajua kilichotokea? Jamaa aliomba bili yake, akalipa kisha akasepa!

Nikaona ni bora niingie kwenye mtandao wa Facebook. Nako nikakuta post nyingi za mashabiki wa Arsenal zikimsifia Alexies Sanchez. Kabla "Likes" hazijafika 10, Swansea walikuwa wamesawazisha. 

Kabla wachangiaji hawajafika watano, Swansea walikuwa wanaongoza. Ghafla Post za Sanchez zikaanza kupotea. Najiuliza kwa nini? Baadaye nagundua kuwa, mshabiki wa Arsenal walikasirika, wakafuta post zao na kisha wakasepa kulala!

Kwa nini wanakasirika? Baadaye nagundua kuwa, hata Cesc Fabregas alikuwa anafunga sana kama Alexies Sanchez, alikuwa anapiga sana pasi za mwisho lakini alipogundua kuwa timu hiyo siku zote inapigania nafasi ya nne, alikasirika sana, akaongeza na hela zake mfukoni kisha, akasepa zake Barcelona. 

Badaye namkumbuka  mshambuliaji, Roben Van Persie kuwa na yeye alifunga sana, alipiga sana pasi za mwisho lakini mwishowe, alikasirika sana na akasepa zake Manchester United.

Unadhani itakuwa na faida gani kama timu itamaliza kwenye nafasi ya nne huku Sanchez akiibuka mfungaji bora? Jibu ni hakuna. Arsenal haikumuhitaji Sanchez ili kumaliza kwenye nafasi ya nne. Malengo ya Arsenal pengine ni angalau kufika nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya na kutwaa ubingwa wa ligi kuu.

Wakati ukiyatafakari hayo, upande wako wa pili unagundua kuwa beki wa kati siku hizi ni Nacho Monreal, Kiungo mkabaji ni Methieu Flamini na ikitokea Arsenal inataka kuongeza nguvu ya washambuliaji kwenye  mechi kama ya jana, unaona kocha Arsene Wenger anamtazama kaka Sanogo kama mkombozi wake!

Nafahamu kama Laurent Conscienly na Methieu Debuchy ni majeruhi lakini, timu inayohitaji kufika angalau nusu Fainali ya Uefa na kutwaa Ubingwa wa ligi kuu, inahitaji kuwa na beki angalau watatu wa kati ambao uwezo wao haupishani sana. 

Inahitaji pia watu kama hao kwenye safu ya kiungo na kwenye safu ya ushambuliaji. Ukitazama pale Arsenal, unakasirika sana kisha unalipa bili na kusepa zako. 

Wenger anafahamu tatizo la Gunners na ndiyo maana leo ukisikia Arsenal wanamtaka Semi Khedira, kesho utasikia wanamtaka beki wa Borussia Dortmund, Mats Hummels. Hii ni ishara tosha kuwa, uongozi unafahamu sehemu timu yao inapopwaya. 

Wachezaji wa kutatua matatizo ya Arsenal, huwa wanaishia magazetini tu. Ukisikia Arsenal imemsajili Marco Reus, unaweza kufurahi kutokana na ubora wa mchezaji huyo na kuamini kwamba timu iko tayari kwa ushindani na kusahau kuwa, tatizo la Arsenal halitatuliwi na mchezaji aina ya Marco Reus.

Mechi zote nilizotaja hapo juu, Alexies Sanchez alifunga goli lakini, baada ya dakika 90 alitoka anatingisha kichwa. Inasikitisha kumuona Sanchez jana akitoka anasononeka lakini unadhani atafanyaje? Timu zilitomtaka wakati akiwa Barcelona, ni Arsenal na Liverpool. Hali ya timu zote hizo kwa sasa ni Pipa na Mfuniko.

Nilikuwepo pia Uhuru Peak wakati  Arsenal wakiisambaratisha Galatasaray huku Sanchez akifunga bao moja na kutengeneza mengine mawili, Nilikuwepo pia wakati Sanchez akiwaadhibu Wes Brown na kipa wake, Vito Manone na Inshallah, nitaendelea kuwepo Uhuru Peak kama ambavyo Arsenal wanavyoendelea kupigania nafasi yao ile ile kila siku.

Ukitazama mapungufu ya Liverpool na Manchester United, unagundua kuwa, Arsenal wanaweza kutatua kirahisi kuliko timu nyingine lakini, Wenger ana amini wachezaji wake wataiva hata kama hachochei kuni. Mzee anapenda sana nafasi ya nne kama mimi ninavyopenda kukaa Uhuru Peak! safi sana.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!