Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 January 2015
Sunday, January 18, 2015

Yanga mambo si shwari!


Na Oscar Oscar Jr

Mabingwa mara 24 wa kihistoria wa Ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga jana ilijikuta kwenye hali ngumu baada ya kulazimishwa sare tasa na maafande wa Jeshi la kujenga Taifa, timu ya Ruvu Shooting kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini  Dar es Salaam.

Baada ya kutolewa kwenye michuano ya Mapinduzi katika hatua ya robo fainali, timu hiyo ilitarajiwa kurejea kwenye ligi kuu kwa kishindo lakini mambo yamekuwa kinyume na matarajio ya wapenzi wa klabu hiyo. 

Yanga walicheza vizuri sana huku wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini kukosa umakini kwa safu yao ya ushambuliaji kulipelekea kupatikana kwa sare hiyo isiyokuwa na magoli.

Ruvu shooting ambao waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kichapo walichopewa na Mgambo JKT kule mkoani Tanga, jana waliweza kuwaheshimu Yanga na kukaba kwa nidhamu ya hali ya juu.

Licha ya ukuta wa Ruvu Shooting kufanya makosa mengi hususani kipindi cha kwanza, golikipa wa Wanajeshi hao alikuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kuokoa michomo mingi iliyokuwa na mwelekeo wa kuzaa magoli.

Simoni Msuva ambaye kwa msimu huu ndiye anayeonekana mchezaji bora wa klabu hiyo, jana hakuwa kwenye ubora wake baada ya kukosa nafasi nyingi za kufunga. 

Mshambuliaji Amis Tambwe na Kpah Sherman nao wakishindwa kutamba licha ya kupata nafasi kadhaa ambazo kama zingetumika vizuri, Yanga wengeliweza kuchomoza na ushindi.

Deogratius Munishi hatimaye amepoteza nafasi ya kuwa kipa namba moja wa Wanajangwani hao baada ya kocha Hans Van Der Pluijm kuonyesha imani kubwa kwa Ally Mustapha maarufu kwa jina la Barthezi.

Tangu kuanza kwa michuano ya Mapinduzi iliyorindima visiwani Zanzibar, Barthez amerejea rasmi langoni na jana alianza tena kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa ligi kuu baada ya kukosa nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Matokeo hayo yanawaacha Yanga wakiwa na alama 15 na Ruvu Shooting wakitimiza alama 12 kwenye msimamo wa ligi kuu ambao unaongozwa na Azam Fc ambao hapo jana walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Baada ya ushindi huo kwa Azam Fc, wamefanikiwa kutimiza alama 17 wakifuatiwa na Mtibwa Sugar wenye 16 sambamba na JKT Ruvu ambao leo wanakutana ndani ya Azam Complex majira ya saa 10:30 Jioni.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!