Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 December 2014
Thursday, December 18, 2014

NIFIKIRIAVYO: ASANTE NA KWAHERI THIERRY HENRY.


Na Chikoti Cico


Mshairi na Mwandishi wa vitabu kutoka nchini Marekani Maya Angelou katika moja ya mistari ya mashahiri yake aliwahi kuandika “People will forget what you said, people will forget what you did but people will never forget how you made them feel” 

Akimaanisha“watu watasahau ulichokisema,watu watasahau ulichokifanya lakini kamwe watu hawatasahau ulivyowafanya wajiskie” Maneno hayo ya Mshahiri Maya yanaakisi maisha ya Thierry Henry moja ya washambuliaji bora kuwahi kutokea duniani hasa kwenye historia ya ligi kuu nchini Uingereza ambako ndipo dunia iliweza kuujua umahiri na ubora wake katika kupachika mabao.

Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Ufaransa ametangaza kustaafu soka baada ya kuzichezea kwa mafanikio makubwa timu za Monaco, Juventus, Arsenal, Barcelona na New York Red Bulls huku akiichezea Arsenal kwa miaka nane ikiwa ni muda mrefu zaidi kuliko timu nyingine zote alizozichezea.

Katika msimu wa mwaka 2009/2010 kwenye mechi kati ya Arsenal dhidi ya Manchester United Henry aliifungia Arsenal goli akiwa umbali wa yadi 20 kutokea golini na kuipa Arsenal ushindi wa goli 1-0, kipa wa United wakati huo alikuwa Fabiam Barthez.

Baada ya mchezo huo kocha wa Manchester United kwa wakati huo Sir Alex Ferguson akiongelea goli hilo alisema “huwezi kufanya chochote kwa goli kama lile, sikuweza kuamini, Highbury na Arsene wangeweza kuamini” hayo ni maneno mazito lakini kwa kifupi yalitoa picha ya ubora wa Henry kwenye kufumania nyavu.

 Henry anakuwa moja ya washambuliaji walioweza kunyakua vikombe vyote kwenye ngazi ya klabu huku akishinda makombe ya ligi za Ufaransa, Uingereza, Hispania na pia kunyakua kombe la ligi ya mabingwa Ulaya na timu ya Barcelona.

Pia Henry aliweza kunyakua kombe la Dunia na timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 1998 baada ya kuifunga Brazili kwa magoli 3-0 kwenye fainali ya michuano hiyo huku Henry akiibuka mfungaji bora kwa timu ya Ufaransa baada ya kufunga jumla ya magoli matatu kwenye fainali hizo hakika hapa pia aliwafanya wananchi wa Ufaransa kujiskia vizuri.

Mpaka anaondoka Arsenal aliweza kuifungia magoli 228 huku akiichezea michezo 376 na kunyakua kombe la ligi mara mbili, kombe la FA mara tatu na kuchukua Ngao ya Jamii mara mbili, hakika aliwafanya mashabiki wa Arsenal wajiskie vizuri kwa magoli yake uwanjani mpaka kufikia kujengewa sanamu karibu na uwanja wa Emirates.

Umahiri wa Henry katika ufungaji wa magoli ulidhihirika karibu kila ligi aliyocheza kwani alifunga jumla ya magoli 411 kwa timu zote alizozichezea huku akiibuka na tuzo mbalimbali zikiwemo za ufungaji bora na uchezaji bora. 

Martin Keown nahodha wa zamani wa Arsenal aliwahi kumwambia Henry kwamba “Nitaweza kuwaambia wajukuu zangu kwamba niliwahi kucheza nawe, na ni mara chache huwa nawapongeza watu”

Maneno yaliyodhihirisha jinsi ambavyo wachezaji wengi walimhusudu Thierry Henry na kuna taarifa kwamba wakati flani uongozi wa Arsenal ulimtishia Henry kwamba ataanza kulipia jezi zake mwenyewe baada ya kuwa wachezaji wengi walitaka kubadilishana nae jezi uwanjani moja ya matendo yanaonyesha jinsi gani Henry alikubali hata na wachezaji wenzake uwanjani. 

Leo Henry anapoamua kustaafu, dunia ya soka itabaki na kumbukumbu ya pekee juu ya umahiri wake uwanjani lakini zaidi sana atakumbukwa sio kwa aliyoyasema wala kwa aliyoyafanya bali kwa jinsi alivyowafanya mashabiki wa soka duniani wajiskie. Mwisho binafsi naomba niseme.

 “ASANTE NA KWAHERI HENRY”.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!