Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 November 2014
Friday, November 07, 2014

Mechi za Jumamosi hii Ligi kuu Tanzania bara.


Na Oscar Oscar Jr

Ligi kuu Tanzania bara inaingia kwenye mzunguko wa saba wiki hii ambapo mechi tano zinatarajiwa kupigwa siku ya Jumamosi kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini na michezo migine miwili, ikitarajiwa kupigwa siku ya Jumapili.

Baada ya kukosa ubingwa kwenye mechi tatu walizocheza msimu hu nyumbani, Stand United watawakaribisha timu ya Mbeya City kutoka mkoa wa Mbeya. 

Stand United wanakamata nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi sita huku, Mbeya City wao wapo nafasi ya mwisho wakiwa na alama tano pekee.

Mbeya City waliomaliza kwenye nafasi ya tatu msimu uliopita, hawajaanza vema msimu huu na mpaka sasa wamefunga magoli mawili tu huku safu yao ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao matano. 

Kwa Upande wa Stand United, wao wamepoteza mechi mbili pekee na wanaonyesha matumaini kwenye safu yao ya ushambuliaji ambapo wamefunga mabao tisa mpaka sasa.

Mechi nyingine itapigwa Dar es Salaam ambapo timu ya Yanga itawaalika timu ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa. Yanga tayari wameshapoteza michezo miwili huku wakitarajia kucheza bila Nahodha wao, Nadir Haroub aliyepigwa kadi nyekundu mchezo uliopigwa Kaitaba pale timu hiyo ilipofungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Mgambo ni timu ambayo haitabiriki na wiki iliyopita, ilifanikiwa kuilaza Mbeya City kwa mabao 2-1 kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga. 

Tayari Mgambo wako kwenye nafasi ya sita wakiwa na alama tisa na ushindi katika mchezo huo, utawafanya wasogee kwenye timu nne za juu.

Yanga kwa sasa, wapo kwenye nafasi ya nne wakiwa na alama 10 ambazo ni sawa na timu ya Azam. Ushindi kwenye mchezo huo, utawarejeshe kwenye nafasi nzuri ya kupigania ubingwa msimu huu. Bado safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, haijaonyesha cheche zake kwani mpaka sasa, wamefunga mabao saba pekee.

Katika Uwanja wa Chamazi Complex, utapigwa mchezo mkali kati ya Azam Fc dhidi ya Coastal Union. Coastal Union wanashika nafasi ya pili mpaka sasa kwenye msimamo wa igi kuu baada ya kujikusanyia alama 11huku, Azam wao wakisalia kwenye nafasi ya tatu wakiwa na alama 10 baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo.

Coastal Union ambao wamefunga magoli nane mpaka sasa, watakutana na safu ya Ulinzi ya Azama ambayo imeruhusu mabao matatu pekee kwenye mechi sita walizocheza msimu huu. 

Azam ni mabingwa watetezi wa ligi kuu, kama watapoteza mchezo huo ni wazi kuwa hawatokuwa kwenye hali nzuri kisaikolojia. Timu zote zinaonekana kuwa na maandalizi mazuri na wapenzi wa soka nchini wanatarajia kupata burudani.

Baada ya kuwasimamisha vigogo wa ligi kuu Tanzania bara, klabu za Simba na Yanga, timu ya Mtibwa Sugar wanajiandaa kuwakaribisha wakatamiwa wenzao timu ya Kagera Sugar kwenye mashamba ya miwa kule Manungu Turiani mkoani Morogoro kwenye mchezo wa ligi kuu.

Mtibwa Sugar ndiyo vinara wa ligi hiyo baada ya kutoka sare ya 1-1 na timu ya Simba wiki iliyopita, walitimiza alama 14 huku wakiwa wamefunga mabao tisa na kuruhusu nyavu zao kutikiswa kwa mabao mawili pekee kwenye mechi sita ambazo wamecheza msimu huu.

Wakati Mtibwa wakiwasimamisha Simba wiki iliyopita, Kagera Sugar nao walifanya kazi kubwa ya kuwachapa watoto wa kocha Maximo, timu ya Yanga kwa bao 1-0. 

Kila timu iko kwenye wakati mzuri wa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo ingawa Mtibwa, wameonekana kutumia vema uwanja wao wa Nyumbani.

Na mechi ya mwisho siku hiyo, itapigwa kwenye dimba la Jamhuri Morogoro ambapo timu mbili za majeshi zitakutana. Polis Moro wanajiandaa kuwakaribisha ndugu zao wa jeshi la Magereza, timu ya Tanzania Prisons. 

Polis Moro kwa sasa, wanashika nafasi ya 12 wakiwa na alama sita huku Tanzania Prisons wao wakiwa nafasi ya 10 japokuwa nao wana alama sita pekee.

Polis Moro walipata ushindi wao wa kwanza wiki iliyopita wakiwachapa bao 2-1 JKT Ruvu huku Tanzania Prisons, wakitoka sare ya 1-1 na Stand United. 

Mchezo huu utakuwa wa ushindani kwani kila timu inataka kujiweka kwenye mazingira salama kabla mzunguko wa kwanza wa ligi kuu kumalizika. Mechi za Simba vs Ruvu Shooting na ule wa Jkt Ruvu vs Ndanda, zinatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!