Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 December 2014
Tuesday, December 02, 2014

SSERUNKUMA USISAHAU KUZUNGUMZA NA TAMBWE.


Na Chikoti Cico

Baada ya ligi kuu nchini Tanzania kusimama huku timu zikiwa na nafasi ya kufanya usajili, Wekundu wa Msimbazi Simba wamefanya usajili wa mshambuliaji wa Uganda, Dan Sserunkuma kutoka timu ya Gor Mahia ya Kenya.

Mshambuliaji huyo ambaye ametajwa na kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Sredejovin Milutin Micho kama mshambuliaji bora kwasasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki anatarajia kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu ya Simba.

Kabla hatujaanza kuona umahiri wa Sserunkuma kwenye ligi kuu Tanzania Bara, ningependa kumkumbusha jambo moja la muhimu mchezaji huyu ambaye tayari ashamaliza kufanya vipimo vya afya kabla hajaanza kuonyesha makali yake.

Ningependa kumkumbusha Ssenkuma kuzungumza na Amissi Tambwe, anachoweza kufanya ni kumchukua Tambwe na kwenda nae kwenye hoteli moja ya kifahari wakati flani wa jioni baada ya mazoezi ya Simba na kuagiza chakula cha jioni sambamba na mvinyo na kuanza kufanya mazungumzo yatakayokuwa kwenye mfumo wa maswali ambayo yatakuwa machache lakini ya msingi.

Kwanza kabisa Sserunkuma baada ya kunywa funda moja la mvinyo ambao labda unaweza kuwa mvinyo aina ya St Anne ama Dodoma Wine, angeanza kwa kumpongeza Tambwe kwa kuibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Kagame na msimu uliopita wa ligi kuu nchini Tanzania huku akifunga magoli 19.

Hapo hapo anatakiwa kumuuliza vipi mfungaji bora wa msimu uliopita mpaka sasa una goli moja tu?

Hapa majibu ya Tambwe yanaweza kuwa kwamba aliumia na hivyo hakuwa fiti msimu ulipoanza lakini kama Sserunkuma akimdadisi zaidi Tambwe, anaweza kupewa majibu mazito na ambayo yatamshangaza zaidi.

Naamini Tambwe ataeleza jinsi gani toka msimu uliopita kuisha, hakuna ambaye ameonyesha kumjali tena wala kumheshimu mshambuliaji huyo na hakuna kiongozi anayekumbuka kama alifunga magoli 19 na kuisaidia Simba kushika nafasi ya nne msimu uliopita.

Majibu hayo yanaweza kumtisha Sserunkuma lakini ndiyo ukweli ambao anatakiwa kuufahamu kuhusu soka letu lenye siasa za kila namna.

Hapo namini lazima ashushie majibu hayo kwa funda lingine la mvinyo huku akimwangalia Tambwe kwa umakini kama anachosema ni kweli ama la na hapo atagundua ukweli wa asemayo.

Na baada ya muhudumu kuleta chakula na kuwakaribisha, Sserunkuma ataweza kumwuliza swali lingine Tambwe kwamba hana hofu na ujio wake kwenye timu hiyo?

Na bila kutafuna maneno, Tambwe anaweza kumjibu kwamba ndiyo anamhofia na siyo kwasababu za kimpira bali sababu za siasa za mpira.

Tambwe atamweleza jinsi ujio wa Okwi ulivyokuwa wa mbwembwe nyingi na kufanya mchango wake kwenye timu kusahaulika ndani ya kipindi kifupi hivyo kwa ujio wake Sserunkuma, ndiyo kabisa atapoteza thamani kwa viongozi waliomsajili.

Hapa Sserunkuma ataweza kutabasamu moyoni lakini pia ataweza kujua kwamba ni jinsi gani ujio wa mchezaji mpya hasa kutoka nje ya nchi unavyochukuliwa kwa uzito na viongozi wa klabu za Tanzania bila kujali mchango wa wachezaji waliopo.

Huku chakula kikikaribia kuisha, Sserunkuma ataweza kumuuliza Tambwe swali la mwisho kwamba, kuna umuhimu gani katika kuwafunga Yanga kwa mashabiki na viongozi wa Simba?

Hapa kabla ya Tambwe kujibu swali hilo, atamalizia mvinyo yake kwenye glasi na kutabasamu kisha kumwangalia usoni Sserunkuma na kusema, “kama unataka ujiskie kama unaishi peponi na kupendwa na kila mtu ambaye anahusiana na timu ya Simba basi wafunge Yanga”

kisha atanyamaza na kuendelea “lakini pia usisahau kinyume cha majibu hayo” bila kuongeza neno lolote Tambwe atamshukuru kwa chakula cha jioni mchezaji mwenzake huyo wa Samba na kuagana nae.

Na katika jibu hilo ndipo Sserunkuma atakapomalizia fundo la mwisho la mvinyo kwenye glasi na kushusha pumzi ndefu huku akielewa sasa kipimo cha ubora wake sio tu kuifunga Azam, mtibwa wala Mbeya City bali Yanga na kwa kuifunga Yanga ndipo atakapojua kama atashangiliwa ama kubezwa.

NAWASILISHA.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!