Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 November 2014
Friday, November 07, 2014

Mechi zote za EPL Jumamosi hii


Na Oscar Oscar Jr

Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kutimua vumbi Jumamosi hii ambapo, viwanja sita vinatarajiwa kuwaka moto huku macho ya watu wengi yakipelekwa kwenye dimba la Anfield ambako Liverpool watawakaribisha vinara Chelsea kwenye mchezo utakaopigwa majira ya saa 9:45 Alasiri.

Liverpool wanaoshika nafasi ya saba wakiwa na alama 14, tayari wamepoteza mechi nne za ligi kuu msimu huu na wanaonekana kudhamiria kufanya vizuri kwenye mechi yao na Chelsea baada ya kupumzisha wachezaji wao saba wa kikosi cha kwanza kwenye mchezo wao wa klabu bingwa Ulaya walipocheza na Real Mdrid na kulala kwa bao 1-0 ugenini.

Chelsea ndiyo timu ambayo haijafungwa hata mchezo mmoja mpaka sasa kwenye ligi kuu ya Uingereza na ni wazi kuwa,  watataka kuendeleza rekodi hiyo watakapokutana na Liverpool Anfield. 

Chelsea msimu huu, imeonekana kuwa tishio baada ya usajili wa Diego Coasta na Cesc Fabregas kuwa na tija ukilinganisha na usajili wa Liverpool ambao haujaonekana kuisaidia timu kwa kiasi kikubwa mpaka sasa.

Katika dimba la Old Trafford, Manchester United watawakaribisha timu ya Crystal Palace kwenye mchezo utakaopigwa majira ya saa 12 Jioni. 

Manchester United baada ya kupoteza mchezo wao uliyopita walipocheza na mahasimu wao Manchester City, watataka kujiimarisha kwa kuibuka na ushindi dhdi ya Crystal Palace ambao wanashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi kuu huku wakiwa na alama tisa pekee.

Crystal Palace ni moja kati ya timu zenye safu mbovu ya ulinzi na mpaka sasa, wameruhusu kufungwa magoli 19 ambayo ni sawa na timu ya Burnley inayokamata nafasi ya mwisho (20). 

Manchester United ambao wako kwenye nafasi ya 10 wakiwa na alama 13, wanahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kumaliza kwenye moja ya nafasi nne za juu.

Mechi nyingine kali, itakuwa pale St.Marry's ambapo timu ya Southampton itawakaribisha Leicester City mchezo utakaopigwa majira ya saa 12:00 Jioni. 

Southampton mpaka sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu huku wakiwa na alama 22 na kupoteza mechi mbili pekee msimu huu.

Leicester City wako kwenye nafasi ya 18 wakiwa na alama tisa pekee na kichapo kwenye mchezo huo, kinaweza kuwaweka pabaya kwani wanaweza kushuka hadi kwenye nafasi ya 20. 

Wakati beki ya Leicester City ikiruhusu magoli 16 mpaka sasa, safu ya ushambuliaji ya Southampton imeshafunga mabao 21. Hii itakuwa ni vita kati ya mabeki wa Leicester City dhidi ya washambuliaji wa Southampton.

Southampton ni timu ambayo imewashangaza mashabiki wengi kutokana na matokeo mazuri wanayopata mpaka sasa huku, ikiondokewa na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza msimu uliopita zaidi ya watano. 

Mshambuliaji, Graziano Pelle na kocha Ronald Koeman, wanastahili pongezi kwa mapinduzi makubwa waliyoonyesha mpaka sasa.

Mechi nyingine, itakuwa kati ya West Ham United dhidi ya Aston Villa mchezo ambao utapigwa majira ya saa 12:00 kwenye dimba la Boleyn. 

West Ham United wako kwenye nafasi ya tano wakiwa na alama 17 ambazo ni sawa na timu ya Arsenal na ushindi kwenye mchezo huo, utawapeleka kwenye timu nne za juu.

Aston Villa nao wapo kwenye nafasi ya 16 huku wakiwa alama 10 na kama watapata ushindi, wanaweza kusogea hadi kwenye nafasi ya 12. 

Mpaka sasa Aston Villa na Burnely ndiyo timu zenye mabao machache ya kufunga EPL (5) huku Villa wao wakiruhusu kufungwa magoli 16.

Mechi nyingine itakayopigwa saa 12: 00 Jioni, itakuwa kati ya Barnley wanaoshika nafasi ya mwisho wakiwa na pointi nne dhidi ya Hull City mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Turf Moor.

Hull City ambao wanashika nafasi ya 14, watahitaji kusaka ushindi wao wa tatu msimu huu baada ya kushuka dimbani mara 10 huku wakishinda michezo miwili pekee. 

Bado hawako vizuri kwenye safu yao ya ulinzi ambapo mpaka sasa, wamesharuhusu kufungwa mabao 14 licha ya washambuliaji wao kufunga mabao 13. 

Burnely wao ndiyo timu pekee ambayo haijashinda hata mchezo mmoja na watakuwa na hamu ya kufanya hivyo Jumamosi hii mbele ya mashabiki wao.

Katika dimba la Louftus Road, vijana wa kocha Harry Redknapp watakuwa wenyeji wa bingwa mtetezi, Manchester City kwenye mchezo unaotarajiwa kuanza majira ya saa 2:30 Usiku. 

QPR walikuwa na mchezo mzuri sana wiki iliyopita dhidi ya Chelsea, licha ya kuwa hawakupata alama yoyote kwa kuchapwa bao 2-1.

Manchester City baada ya kuchechemea kwenye klabu bingwa Ulaya baada ya kuchapwa na timu ya CSKA Moscow bao 2-1 huku Kiungo Yaya Toure na Fernandinho wakipewa kadi nyekundu, watalazimika kusahau matokeo hayo na kurejea kwenye mchezo huu wakiwa na nia ya kutetea ubingwa wao walioutwaa msimu uliopita. 

Manchester City wako kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu wakiwa na alama 20 huku QPR, wao wakisalia kwenye nafasi ya 19 wakiwa na alama saba pekee. 

Mpaka sasa QPR ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi EPL (20) na Sergio Kun Aguero wa klabu ya Man City, ndiye mshambuliaji anayeongoza kwa upachikaji wa mabao (10).




0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!