Searching...
Image and video hosting by TinyPic
17 November 2014
Monday, November 17, 2014

Mario Balotelli Mlaumu hapa, siyo pale.



NA MARKUS MPANGALA 

WAPO washambuliaji watatu katika kikosi cha Liverpool ambao wanakipiga kwa miezi kadhaa sasa. Ni Mario Balotelli, Fabio Borini na Rickie Lambert. Wote kwa pamoja wametumia dakika 888 kuitafutia mabao klabu ya Liverpool. 

 Daniel Sturridge ni majeruhi, huenda akarejea dimbani wikiendi ijayo dhidi ya Crystal Palace. Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers ni fundi mzuri wa kandanda. Kitu kimoja anachokifanya ni kuamini ushindi kupitia soka la burudani. 

Eneo moja nisilokubaliana naye, ni kwanini alimua kumpiga bei Stewart Downing. Falsafa yake ya kupiga pasi fupi za haraka na kuburudisha ni kitu ambacho Stewart Downing angeweza kumksaidia. 

Labda tatizo ni umri wa Downing. Liverpool ikicheza watu wanaelekeza macho yao kwa Mario Balotelli. Wengine wanamlaumu Brendan kwamba hakutakiwa kumsajili Balotelli. 

Binafsi nilishangaa kumsajili Balotelli, upo wakati nilisema anapoteza muda kutegemea mchezaji ambaye hayupo makini na nidhamu yake. Lakini pia nilimkumbuka Daniel Sturridge alipokuwa Chelsea. Sturridge ana kipiaji cha soka. 

Ni fundi mzuri ambaye wakati mwingine nilidhani angecheza winga au beki wa kushoto. Lakini Brendan Rodgers ameendelea kumwamini, akamtengeneza na kuwa staa wa England. 

Chelsea walitamani kumrudisha kundini, labda hata Manchester City alikoanzia soka wangetamani. Lakini Brenadn Rodgers aliamini Sturridge ni mshambuliaji sahihi kwa mbinu zake. 

Sturridge analo tatizo moja tu; uchoyo. Kuna wakati hatoi nafasi katika muda sahihi, lakini anaweza kusahihisha makosa yake kwa kufunga bao zuri na kuipa ushindi Liverpool. 

 Hii ni bahati kwake, na amefanikiwa kukituliza kichwa chake kucheza mpira. Mara nyingi nimewasikia waingereza wanavyomshambulia, lakini ndani ya wiki moja naona tayari wanaanza kuona kwa macho tofauti. Binafsi nimekiona anachokitafuta Brendan Rodgers kwa Mario Balotelli. 

Kinachochelewesha ni kumpata mshambuliaji wa pili ambaye atatengeneza ‘kombinesheni’ ya uhakika. Sifa moja ya Balotelli ni uimara wa mwili wake na inadaiwa si mchezaji wa kupata majeraha mara kwa mara. 

Kwa mtazamo wangu Balotelli hakuwahi kucheza mpira wa uhakika katika timu yoyote kama anavyofanya akiwa Liverpool. 

Akiwa Inter Milan, nakumbuka mechi ya nusu fainali dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa. Mashabiki wabaguzi walimzomea, naye kwa hasira akapiga shuti kuelekea walipo badala ya kupiga langoni. 

Jose Mourinho hakuvumilia alimkaripia na ugomvi ukazidi. Balotelli akiwa Manchester City sikuwahi kuona kama yupo ‘serious’ na soka. 

Hakuwa akicheza muda mwingi wa mchezo. Hakuwa mshambuliaji mwenye juhudi zozote na mara nyingi alikuwa mtu wa vituko badala ya soka. Akiwa Man City nilimuona mchezaji ambaye alikosa usimamizi kama wa Brendan Rodgers wa Liverpool. 

Sasa tofauti yake ni ipi? Mario Balotelli wa sasa anaweza kukimbia eneo kubwa la uwanja ndani ya kikosi cha Liverpool. Balotelli anakaba, anatafuta nafasi, anatengeneza nafasi, anafanya juhudi kwa ajili ya timu siyo binafsi kama alivyokuwa Man City, AC Milan na Inter. 

Balotelli wa Brendan Rodgers anatumia muda mwingine kucheza kwa ajili ya timu, anaweza kukosa mabao, lakini anajitahidi kuifanya Liverpool icheze mpira. 

Kila mechi ya Liverpool naangalia eneo alilopo Balotelli. Najiuliza hii akili Balotelli aliipata lini? Balotelli anacheza huku na huko, anachezewa rafu, anafanyiwa ubabe, anachokozwa, lakini yuko kimya. 

Ukorofi wa Balotelli umepungua, vituko ni adimu ndani ya uwanjani. Ni wazi Balotelli anacheza soka sasa, kwamba yuko chini ya watu makini zaidi kuliko ‘baba yake’ wa soka Roberto Mancini. 

Brendan Rodgers anakitafuta kitu miguuni mwa Balotelli, na hakika kwa jinsi anavyoifanya Liverpool anaweza kukipata. Kuna mambo mengi chanya kwa Balotelli na yanamvuta mtu makini kama mimi kumwangalia anafanya nini uwanjani. 

Tatizo linalowakabili Liverpool, ni kumtumia Balotelli kama alivyo. Tatizo jingine kwa Balotelli ni kushindwa kuitumia Liverpool kumfanya awe bora zaidi. 

Kwamba Liverpool inapomhitaji Balotelli inatakiwa kuangalia staili yake ya kucheza. Wakati Balotelli anapotaka kuidhihirishia dunia sasa yuko ‘bize’ na mpira, anashindwa kuitumia staili ya Liverpool kuipa mafanikio. Kuna dawa moja tu; mshambuliaji wa pili ambaye atakuwa karibu na Balotelli. 

Mechi ya Real Madrid pale Bernabeu hakupangwa, lakini Liverpool ilicheza soka la La Liga, na lilionesha kiu ya Brendan Rodgers kufundisha soka Hispania. Karibu sana Brendan. Sasa kama Liverpool ikipanga kutumia washambuliaji wawili, Tatizo hasa itakuwa kiungo mkabaji. 

Kama watampanga Balotelli, basi wanatakiwa kuwa na viungo wawili washambuliaji, Joe Allen na Philipe Coutinho pamoja na Sterling kumzunguka Balotelli. 

Sturridge anarudi, nadhani ni wakati wa kuona watafanya nini pamoja na Balotelli. Unaweza kumlaumu Balotelli hafungi mabao, usimlaumu pale anapojitolea kwa ajili ya timu. Anavutia siku hizi, lakini hatumtaki pale Real Madrid! Haaaaah!

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!