Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 October 2014
Tuesday, October 21, 2014

Usajili wa wachezaji una yakuzingatia.



Na Samuel Samuel

Timu inatakiwa isajili wachezaji 15 ambao wako chini ya umri wa miaka 25. Ukiwa na wachezaji wengi wenye kuanzia miaka 18 hadi 25 basi klabu ina uhakika wa kukaa na wachezaji hao kwa zaidi ya miaka sita. 

Hali hiyo itawafanya wajuane vizuri, wakue pamoja na kujenga uzalendo katika klabu husika. Yanga ya mwaka 1992, Simba ya 1993 na Sigara ya kina Beni Luoga, ni matunda ya mfumo huu.

Pia usajili unatakiwa kuangalia wakongwe wenye nidhamu nzuri ambao watasimamia nidhamu ya vijana na wanatakiwa kuwa na skills za kutosha ili wachezaji chipukizi wajifunze toka kwao na ni jambo zuri kama timu haitosajili zaidi ya wachezaji 10  kwa msimu au kuacha idadi kubwa ya wachezaji kila msimu.

Unaposajili wachezaji wengi wapya, jua utaanza kujenga msingi upya mpaka waje wakae sawa si leo wala kesho. Simba imesajili wachezaji wapya wengi mwaka huu hali hiyo inawapa wakati mgumu kupata matokeo mazuri. 

Bado chipukizi kama Maguri, Isiaka , mohamed Hussein , Manyika na baadhi ya wakongwe wapya kama Kisiga, Kwizera hawajakaa sawa . Yanga imeacha wachezaji 11 iliyokuwa nao msimu uliopita nao bado hawajatulia. 

Unapozungumzia usajili lazima kuliangalia benchi la ufundi pia. Klabu nyingi nchini zinabadili sana makocha. Hii ni sawa na gari kuwa na madereva wengi kwa wakati mmoja. Kila kocha anakuja na falsafa zake. Kila siku timu inakuwa kama inaanza moja.

Klabu zinatakiwa kupata makocha wazuri wenye uwezo wa kukaa na timu kwa mafanikio si chini ya miaka sita mpaka kumi. Man United ilifanikiwa sana chini ya kocha Sir Alex Ferguson kwa staili hili. Ndanda imefukuza kocha katika mechi nne tu! Hapo utaona tatizo la kukosa umakini lilivyo baya. 

Usajili mzuri hufanywa na benchi la ufundi kwa kushirikiana na maskauti wa timu wenye uwezo mzuri wa kumtambua mchezaji mzuri. Ligi inapoendelea kocha hawezi kufika kila mahali.

Kocha anatakiwa kuwa na mikono mingi katika benchi lake la ufundi ambalo litaweza kufuatilia wachezaji sehemu mbali mbali na kumpa taarifa za kutosha kocha kabla ya kumfanyia majaribio mchezaji.

 Mwisho kabisa, klabu ni lazima ziwe na timu za vijana zenye wachezaji wazuri wenye uwezo wa kuhamishiwa timu kubwa kwa 80% sio kuwa na timu ya vijana kukamilisha ratiba tu.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!