Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 October 2014
Tuesday, October 21, 2014

Wafalme wanakuja Anfield!



NA MARKUS MPANGALA 

KWANZA namhurumia sana rafiki yangu Ezekiel Kamwaga ambaye ni shabiki wa Liverpool. Pili, kubwa ya kuichabanga Levante imemalizika mwishoni mwa wiki. Vijana wa Santiago Berbabeu walishinda mabao 5-0. Kwanza Levante imekuwa timu yenye matukio ya kushangaza. 

Kuna wakati inacheza soka la kutisha ndani ya dakika 45 za kwanza na ukishindwa kuifunga muda huo basi kipindi cha pili kinakuwa na kigumu kwako. Levante ni timu ya wastani lakini yenye ushindani mara kadhaa. Baada ya shughuli iliyofanyika mwishoni mwa wiki sasa macho yanaelekea kwenye dimba la Anfield. 

Pambano hilo ni maandalizi pia ya kuwafunga wale vijana wanaotaka kukimbia La Liga kwa sababu ya mikakati ya kutaka kujitenga kutoka Hispania, yaani Barcelona, maana jimbo la Catalunya linataka kujitenga. Tukirudi kwenye pambano baina ya Liverpool na Real Madrid wiki hii ninaweza kusema mambo mengi, lakini itoshe kuelezea machache. 

Liverpool na Real Madrid zinatofautiana sana. Kwanza Liverpool ya Brendan Rodgers si nzuri kucheza ‘counter attack’ kama walivyo Real Madrid. Pili safu ya ulinzi ya Liverpool ina mabeki hodari wawili tu Martin Skrtel na Alberto Moreno. 

Kwa mantiki hiyo napenda kuwawaambia wana Liverpudlian, kuwa wanakutana na timu ambayo inafunga mabao mengi kwenye mchezo wowote pale inapopata nafasi za chache. Niwaambie wana Liverpool kuwa hadi sasa safu ya ushambuliaji wa Real Madrid imefunga mabao 40 tangu kuanza kwa msimu huu. 

Ronaldo amefunga mabao 20, ikiwa na maana mabao 15 ya mechi saba za La Liga. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya amefunga mabao mawili, na mawili kwenye Super Cup, kisha mawili kwa Ureno. Gareth Bale amefunga mabao manne La Liga, moja kwenye Ligi ya Mabingwa na mawili kwa timu ya taifa ya Wales(kuna wasiwasi atakosekana mechi hii).

Karim Benzema amefunga mabao 6, ambapo matatu kwenye La Liga na mawili kwenye Ligi ya Mabingwa na moja kwa timu ya taifa ya Ufaransa. James Rodriguez amefunga mabao matano La Liga (moja ameifungia Colombia). Javier Hernandez amefunga mabao manne. 

Hii ina maana kuwa Real Madrid wana wafungaji wengi zaidi kuliko Liverpool. Katika pambano moja italawalazimu Liverpool kuwalinda Gareth Bale (kama atacheza), James Rodriguez na Karim Benzema ambao huanza kwenye kikosi cha kwanza. 

Chicharito ni mchezaji wa akiba na anaweza kuwa mwiba mwingine kwa Liverpool. Kama kuna kitu kinaitafuna Liverpool basi ni safu ya ushambuliaji kumtegemea Raheem Sterling. Mario Balotelli bado hajaanza kuonesha makali yake pale Anfield. 

Ukiangalia tofauti ya hizi timu lazima utakubali kuwa muziki wa Real Madrid ni mnene na Brendan Rodgers anatakiwa kufanya kazi ya ziada kushinda pambano hilo. Katika pambano la La Liga dhidi ya Levante, Sergio Ramos, Karim Benzema na Raphael Varane walikosekana. 

Lakini kwenye mechi dhidi ya Liverpool vijana hao wote wanategemewa kuwepo dimbani. Real Madrid itashambulia kuanzia kulia (Gareth Bale) na kushoto (Ronaldo na James) pamoja na katikati ya dimba (Benzema na Luka Modric).

Kiungo mkabaji anafahamika atakuwa Toni Kroos ambaye atasaidiwa na Luka Modric mwenye jukumu la kushambulia kupitia katikati ya dimba. Rafiki zangu wa Liverpool wanamtegemea Mario Balotelli? 

UZURI NA UDHAIFU WA LIVERPOOL 

Kama kuna kitu kinawapa matumaini Liverpool ni ushindi wa mwaka 2009 waliopata dhidi ya Real Madrid. Jambo hili kwa namna moja ama nyingine linaonesha jinsi wasivyoangalia tofauti ya vikosi hivi viwili. Ni kweli Liverpool wana faida ya kucheza nyumbani. 

Liverpool wana kocha mzuri Brendan Rodgers. Liverpool wana ufundi wa Philipe Coutinho, Sterling, Moreno, Gerrard na labda Sturridge kama atacheza. Eneo la kiungo la Liverpool lina Lucas Leiva, Joe Allen, na Coutinho. 

Liverpool inacheza soka la burudani na hakika inavutia kuitazama. Adam Lallana anakuwa silaha nyingine ya Liverpool na anaweza kuwa tishio la Real Madrid. Lakini ipo tofauti ndogo, Real Madrid wana sifa moja muhimu sana wana uwezo wa kukimbia uwanjani kwa muda mrefu kuliko Liverpool. 

Real Madrid wataitisha Liverpool kwa kila upande. Nina hakika Liverpool licha ya ufundi wao watakutana na mabingwa wa staili hiyo. Kitu kimoja muhimu kwenye mechi hii, Liverpool imeshinda mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya QPR. 

Bila shaka watakuwa kwenye ari kubwa na utulivu. Lakini Real Madrid haiwezi kumuogopa Balotelli au Adam Lallana. Kitakachowaua Liverpool ni ufundi binafsi walionao Real Madrid. Unataka magoli makali ya vichwa ya Sergio Ramos? Subiri. Unataka mashuti ya Luka Modric? Unataka kumuona mtaalamu wa kutuliza mpira Benzema? Basi nawaomba Liverpool wajiandae kwa burudani. 

NB; Mimi ni shabiki wa Real Madrid(Madridistas), naiheshimu Liverpool ya Ezekiel Kamwaga, ila hamhurumia sana mechi hii.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!