Safari ya Simba kule Sokoine Mbeya
Na Samuel Samuel
Simba Vs Prisons itakuwa moja ya mechi ngumu mwisho wa juma. Mchezo huu unatarajiwa kupigwa jumamosi tarehe 25 katika uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
Simba inakwenda kucheza mechi hiyo baada ya kudroo na watani wao wa jadi Yanga. Timu hizo zilitoka sare tasa ya 0-0 ilihali Prisons ilipokea kichapo cha 2-1 dhidi ya maafande ya JKT Ruvu.
Simba na Prisons mara ya mwisho kukutana katika uwanja wa sokoine, zilitoka sare ya bao 1-1 hali inayoongeza ushindani mkubwa kwenye mechi ya jumamosi.
Simba inakwenda kucheza mechi yake ya kwanza mkoani ikiwa na kumbukumbu mbaya kwani, kwa misimu mitatu mfululizo imekuwa ikishinda mechi zake chache sana za ugenini.
Simba chini ya Patrick Phiri bado haijaonja ladha ya ushindi kwa kutoa sare mechi zote tatu huku, Tanzania Prisons ikiwa imeshinda mechi moja, kwenda sare mchezo mmoja na kupoteza mara mbili.
Simba inahitaji sana ushindi na tayari mechi iliyopita dhidi ya Yanga imeonesha uimara hasa kwenye safu ya ulinzi iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Phiri anakwenda kuivaa Prisons kwa mfumo wa 4-4-2 huku beki yake ikiimarishwa na golikipa Manyika jr ambaye ameonesha uwezo mkubwa mechi ya juzi kwa kuwanyima wakongwe wa ligi Dar Young African.
Safu hiyo ya ulinzi pia ina vijana wazuri kama Hassan Isiaka, Mohamedi Hussein, Miraji na Mkuu wa Kaya Joseph Owino.
Phiri asitegemee mtelemko kwa Prisons timu inayosifika kwenye ligi kwa kuwa na kiungo kizuri kinachoundwa na wachezaji kama Mwangama , Shoji na Maingo.
kocha ya Prisons hatakubali kupoteza mechi mbili mfululizo hali itakayoifanya mechi hiyo kuwa ngumu na ya kuvutia. Prisons ni wanazi wa mfumo wa 4-5-1 na kama unakumbuka waliwapa shida sana Yanga kuibuka na ushindi wa bao 2-1 pale kwenye uwanja wa Taifa.
Prisons itahitaji kulinda heshima ya uwanja wa nyumbani wakati Simba watahitaji kushinda mchezo wao wa kwanza ili kufufua matumaini ya kuufukuzia ubingwa wa ligi unaoshikiliwa na wababe, timu ya Azam.
0 comments:
Post a Comment