Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 October 2014
Monday, October 20, 2014

Mchezo wa Simba vs Yanga kwa kitaalamu zaidi



NA MARKUS MPANGALA
NI mechi ya kwanza kwa watani wa jadi ambao walicheza kwa namna tofauti. Wataalamu wa soka wanasema ukitaka kuelewa zaidi tathimini ya mchezo wowote wa soka ni pale hitimisho linapoonesha namna timu ilivyomiliki mpira, kujaribu kufunga, kufunga, kukaba na kadhalika. 
Katika pambano la Yanga na Simba lililochezwa kwenye uwanja wataifa kulikuwa na kitu kimoja kilochotawala muda mwingi wa mchezo huo; rafu. 
Kitu cha pili ilikuwa mchezo wenye hofu ya kufungwa kwa kila upande. Uchu wa kupata mabao haukuwa wa kiwango cha juu. Washambuliaji walipania, viungo walipania. 
Mabeki walipania. Makocha walipania. Mwishowe unakuta mchezo mzima ulikuwa wa kupaniana na kukosa ushindi. Lakini rafu zinaweza kueleza ukweli kwamba mchezo baina ya Yanga na Simba ulitawaliwa na fujo mno. 
Kwa mujibu wa tathimini iliyooneshwa televisheni ya Azam ni kwamba wachezaji wa Yanga walicheza rafu mara 14 na kupata kona 4 kwa muda wote wa dakika 90. 
Kwa upande wao Simba walicheza rafu mara 18 na kupata kona 1 kwa muda wa wote wa dakika 90. Idadi ya mashuti yaliyolanga lango na yasiyolenga haikuwa kubwa kiasi cha kusema mchezo huo ulikuwa wa kasi au ushindani wa hali ya juu. 

NINI KILICHOTOKEA YANGA, SIMBA
Simba walikuwa na presha kubwa ya kujilinda kutokana na kucheza vibaya tangu mwanzo wa ligi. Yanga walikuwa na presha kubwa hususani kocha wao Marcio Maximo. Pande zote zilitawaliwa na presha ambayo bila shaka ilitakiwa kutulizwa muda wote wa mchezo. 

Maximo kama ilivyo kawaida, alipanga viungo watano katikati ya dimba ambao walikuwa na kazi ya kuwadhibiti Simba. Wakati Simba walikuwa na viungo watatu kabla ya Said Ndemla kuzidiwa na mchezo kisha kutolewa na nafasi yake kuingia Shaban Kisiga. 
Kilichotokea kwa timu hizi ni kukosa uchu wa kupachika bao kutoka na kuwa na mpango wa kujilinda zaidi badala ya kutafuta goli. Kama unapnga viungo watano kisha mshambuliaji mmoja (Jaja), huku viungo hao wakiwa wanalinda zaidi badala ya kushambulia, si kitu rahisi kupachika mabao ya kutosha. 
Kwa Patrick Phiri, Simba ilicheza pasi fupi lakini iliksoa maarifa ya kupenya ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya nahodha stadi Nadir Haroub. 
Emmanuel Okwi alikuwa mchezaji pekee hatari kwa Yanga, lakini hakuwa kwenye mtiririko wa mashambulizi ya Simba. Mara nyingi alionekana kuonesha juhudi binafsi. Kama nilivyosema mwanzo, tathimini inayoonesha rafu za timu hizo inatuletea maana kubwa kwamba Yanga na Simba walipania zaidi mchezo huu. Wachezaji walipania bila kuangalia ari ya kushinda mechi. 
Phiri hakuwa na mpango mbadala kama ilivyokuwa kwa Maximo. Timu zote zilikuwa na lengo moaja ambalo si kupata ushindi bali kulinda heshima zao.
MBINU MBADALA
Engapo Maximo anataka kuifunga Simba inayofundishwa na Patrick Phiri anatakiwa kuhakikisha eneo la kiungo linapunguziwa kazi. 
Kiungo cha Yanga kinatakiwa kusaidia kusogea mbele ya lango la adui si kubaki kujilinda ambako kunasababisha faulo na kuifanya timu ibaki nyuma. 
Phiri kama anataka kuifunga Yanga ya Maximo ni lazima ahakikishe inacheza kwa mtiririko sahihi badala ya ‘one man team’. Okwi alikuwa mtu anaytegemewa kutengeneza nafasi, kutafuta nafasi na kufunga. 
Jambo hili haliwezi kutokea mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga chini ya Haroub na Yondani. Kama Okwi alitakiwa kufanya kazi hizo basi angewekwa nyuma ya washambuliaji wawili ambao wangekuwa na kazi ya kufunga pekee. Yanga inategemea zaidi nguvu ya safu ya kiungo, lakini wanajisahau na kubaki nyuma zaidi hivyo Jaja kushindwa kukaribiwa na pasi za mwisho. 
Jaja hana kasi, hawezi kupambana na mabeki kwahiyo aina yake inatakiwa viungo wataalamu kama Haruna Niyonzima au mshambuliji Hamis Kiiza kucheza kwa ukaribu zaidi.
Nafikiri Maximo anatakiwa kuona namna ya kuwapanga Hamis Kiiza na Jaja mbele, kisha nyuma yao akawapanga Coutinho na Niyonzima. Hii itakuwa na maana winga anatakiwa kuwa mmoja tu Mrisho Ngassa ili kuachana na mfumo wa kutegemea krosi. 
Simba hawana wapiga krosi, hili litakuwa tatizo kwao katika mechi ngumu kama dhidi ya Yanga. Mchezo huu ulijaa fujo sana, rafu nyingi mno kuliko mbinu za kusaka ushindi, ikiwa na maana hata ‘offside’ ni chache wakati zinatakiwa kuwa nyingi kwenye mchezo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!