Anderson arudi kwao Brazil
Na Florence George
Klabu ya soka ya Internacional ya nchini Brazil imefanikiwa kumnasa mchezaji Anderson aliyekuwa anakipiga katika klabu ya Manchester United ya nchini Uingereza na amesaini mkataba wa miaka minne na timu hiyo.
Mchezaji huyo alijiunga na United mwaka 2007 akitokea timu ya FC porto ya nchini Ureno kwa kiasi cha Euro millioni 26.
Anderson alisajiliwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Sir Alex Ferguson na alifanikiwa kuwa mchezaji katika timu ya kwanza"First Eleven" katika miaka minne ya mwanzo na miamba hiyo ya Old Trafford.
Anderson amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara kwa kipindi cha hivi karibuni na ameruhusiwa kuondoka na miamba hiyo ya Old Trafford baada ya kukosa nafasi chini ya kocha Louis Van Gaal na inaripotiwa kuwa mchezaji huyo ameondoka huru(bure).
Msimu uliopita mchezaji huyo alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Fiorentina ya nchini Italia lakini hata hivyo hakuwa na msimu mzuri na timu hiyo.
Msimu huu mchezaji huyo amefanikiwa kuichezea timu hiyo mchezo mmoja ambapo aliingia kama mchezaji wa akiba mwezi August mwaka jana dhidi ya Burnley mchezo ulioisha kwa timu hizo kutoka suluhu(0-0).
Mchezaji huyo amefanikiwa kuichezea United michezo 179 na alikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa ulaya dhidi ya Chelsea mwaka 2008 na kufanikiwa kufunga penati na kuisadia timu hiyo kuibuka mabingwa wa kombe hilo.
Katika kipindi chote alichoichezea United,Anderson alifanikiwa kubeba makombe manne ya ligi kuu nchini Uingereza,kombe moja la klabu bingwa ulaya(UEFA),makombe mawili ya ligi na kombe moja la klabu bingwa dunia.
0 comments:
Post a Comment