Searching...
Image and video hosting by TinyPic
9 January 2015
Friday, January 09, 2015

Uchambuzi: Sunderland vs Liverpool saa 9:45 Alasiri.


Na Chikoti Cico

Viwanja mbalimbali kwenye ligi kuu nchini Uingereza vitawaka moto wikendi hii na katika uwanja wa Stadium of Light wenyeji timu ya Sunderland wataikaribisha Liverpool katika moja ya mechi itakayokuwa ya vuta nikuvute.

Sunderland ambao wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 20 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kupanda juu zaidi kwenye msimamo wa ligi.

Kocha wa Sunderland, Gus Poyet hana wachezaji ambao ni majeruhi ukiachana na kiungo wake mkabaji Lee Cattermole ambaye anasumbuliwa na majeraha ya mtoki lakini anatarajiwa kuwa fiti kwenye mchezo huo dhidi ya Liverpool.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha katika michezo 10 iliyopita ya ligi dhidi ya Liverpool, Sunderland wameshinda mchezo mmoja na kufungwa michezo mitano huku wakitoka sare michezo minne.

Nae winga wa Sunderland Adam Johnson amekuwa na rekodi nzuri ya magoli katika michezo minne iliyopita ambapo amefunga magoli matatu.

Kikosi cha Sunderland kinaweza kuwa hivi: Pantilimon; Vergini, O'Shea, Brown, Van Aanholt; Bridcutt, Larsson, Gomez; Johnson, Wickham, Fletcher.

Kwa upande wa kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers kuelekea mchezo huo atawakosa Adam Lallana, Joe Allen, Glen Johnson, Jon Flanagan na Brad Jones ambao ni majeruhi.

 Pia watakosekana beki, Kolo Toure ambaye ameenda kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika akikosekana, wakati huo huo mshambuliaji wa Liverpool Daniel Sturridge nae atakuwa nje ingawa anakaribia kurejea uwanjani.

Liverpool ambao wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 29 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa nguvu na kutafuta ushindi ili kupata alama tatu muhimu na kufufua matumani ya kuingia kati ya timu nne za juu yaani “top four” kwenye msimamo wa ligi.

Takwimu zinaonyesha katika michezo minane iliyopita ya ligi ambayo Liverpool imecheza kwenye uwanja wa Stadium of Light imeshinda michezo mitano na kufungwa michezo miwili huku ikitoka sare mchezo mmoja.

Kikosi cha Liverpool kinaweza kuwa hivi: Mignolet; Can, Skrtel, Sakho; Henderson, Lucas, Gerrard, Moreno; Coutinho, Sterling, Markovic

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!