Na Chikoti Cico
Mchezo kama huu katika uwanja wa St James Park kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kuu nchini Uingereza ndiyo ulisitisha rekodi ya Chelsea ya kutokufungwa toka kuanza kwa msimu hivyo wikendi hii itakuwa zamu ya Chelsea kulipiza kisasi kwenye uwanja wa Stamford Bridge saa 12:00 Jioni katika mchezo ambao unatazamiwa kuwa wa kusisimua.
Chelsea ambao mpaka sasa wanaongoza ligi pamoja na Manchester City wote wakiwa na alama 46 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kutafuta alamu tatu muhimu ili kuzidi kujichimbia kileleni na kuwakimbia Manchester City.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho hana wachezaji majeruhi kuelekea mchezo huo hivyo wachezaji kama John Terry, Edez Hazard, Cesc Fabregas na Thibaus Courtois ambao waliopumzishwa kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Watford jumapili iliyopita wanatarajiwa kurejea kikosini dhidi ya Newcastle.
Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha John Terry amefunga magoli matatu katika michezo minne iliyopita ya ligi pia Eden Hazard amehusika katika magoli saba katika michezo saba iliyopita ya ligi huku akifunga magoli manne na kutoa pasi tatu za magoli.
Nae kiungo wa Chelsea Cesc Fabregas mpaka sasa ametoa pasi 14 za magoli yaani “goal assist” kuliko mchezaji yoyote kwa msimu uliopita ambapo Steven Gerrard aliongoza kwa kutoa “goal assist” 13.
Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Terry, Cahill, Azpilicueta; Matic, Fabregas; Hazard, Oscar, Willian; Costa
Timu ya Newacastle ambayo inashika nafasi ya 10 ikiwa na alama 27 kwenye msimamo wa ligi itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kocha wa muda baada ya kocha wa zamani wa timu hiyo Alan Pardew kuiacha timu hiyo na kwenda kuifundisha klabu ya Crystal Palace.
Kocha huyo wa muda John Carvers kwenye mchezo huo dhidi ya Chelsea atawakosa Papiss Cisse na Cheick Tiote ambao wameenda kuziwakilisha timu zao za taifa kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Afrika.
Wakati huo huo kipa namba moja wa timu hiyo Tim Krul, anatarajiwa kurejea kikosini baada ya kuwa nje toka Novemba akiwa majeruhi.
Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha Cisse ambaye hatakuwepo kwenye mchezo huo amefunga magoli matano katika michezo sita iliyopita ya ligi huku pia akiifunga Chelsea magoli manne ikiwa ni magoli mengi kuliko timu zingine ambazo ameshawahi kuzifunga.
Kikosi cha Newcastle United kinaweza kuwa hivi: Krul; Santon, Williamson, Coloccini, Dummett; Anita, Colback; Gouffran, Cabella, Sissoko; Perez
0 comments:
Post a Comment