Uchambuzi: Polis Moro vs Stand United
Na Oscar Oscar Jr
Mchezo kati ya Poils Morogoro dhidi ya Stand United wa ligi kuu Tanzania bara, naweza kusema ndiyo itakuwa mechi kubwa ambayo itachezwa leo kwenye dimba la Jamhuri pale mkoani Morogoro.
Baada ya timu za Mtibwa Sugar, Azam, Simba na Yanga kuthibitisha ushiriki wao wa kombe la Mapinduzi, timu zilizosalia zitaendelea na ligi kuu kama kawaida.
Pamoja na kuwa Stand United wanaonekana ni timu ya pili kwenye ligi kuu Tanzania bara kuruhusu kufungwa magoli mengi mpaka sasa (10) ukiachilia mbali Ndanda Fc ambayo imeshafungwa mabao 14, bado ukitazama wanavyocheza na kupanga mashambulizi unashawishika kuwatazama kwa mara nyingine tena.
Stand United ni timu ambayo haijapoteza mchezo wowote ugenini msimu huu. Waliweza kupata ushindi dhidi ya Mgambo JKT kule Tanga na baadaye wamefanikiwa kutoka sare na timu kongwe ugenini kama Simba, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.
Polis ambao wametoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT mechi iliyopita, wameonekana kubadilika na usajili waliofanya wa wazoefu kama Said Bahanuzi aliyekuwa na kikosi cha Yanga utakuwa umeongeza nguvu kikosini.
Polis Morogoro inaonekana kumudu ligi kuu kwani mpaka sasa katika timu zilizopanda daraja, wao ndiyo wanakamata nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu (sita) huku wakiwa pia wameruhusu magoli machache (saba) tofauti na wenzao Stand na Ndanda.
Mara nyingi zinapokutana timu ambazo zinalingana nguvu, tumekuwa tukishuhudia mchezo mzuri na wa wazi na kila timu iko huru kutafuta magoli.
Ukirejelea mchezo baina ya Stand United vs Ndanda Fc, utakubaliana na mimi kuwa ulikuwa mchezo wa wazi na uliweza kuzalisha mabao matano ambapo Ndanda waliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Baada ya Stand United kutoka sare ugenini na vinara wa timu hiyo, Mtibwa Sugar ni wazi pia watakuwa na hali ya kujiamini pale watakapokwenda kuvaana na Polis Morogoro.
Kitendo pia cha Polis cha kupata ushindi mzuri wa bao 2-0 dhidi ya Mgambo, kitakuwa kimeonyesha mwanga kwa kocha Adolf Rishards na kuhakikisha kuwa alama tatu zinabaki morogoro kwa mara nyingine ili kujiweka kwenye mazingira salama.
Uwepo wa mshambuliaji Said Bahanuzi kwenye kikosi cha Polis Morogoro ambaye ametokea klabu ya Yanga na uwepo wa Harouna Chanongo kwa upande wa Stand United ambaye ametokea klabu ya Simba, hii pia itaongeza mvuto na ubora kuelekea kwenye mchezo.
Anyway, hii ni moja kati ya mechi za ligi kuu Tanzania bara ambazo hutakiwa kuzikosa. Nina imani kubwa kuwa huu ni mchezo utakao kuwa na ubora hasa ukizingatia kuwa kila timu inaona kama inauwezo wa kummudu mwenzie licha ya Polis kukamata nafasi ya sita huku Stand United wao wakishika nafasi ya tisa.
0 comments:
Post a Comment