Na Chikoti Cico
Ligi kuu nchini Uingereza inatarajiwa kushika kasi wikendi hii na moja ya mchezo ambao unatarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ni kati ya Chelsea dhidi ya Manchester City mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge kuanzia mida ya saa 2:30 usiku.
Klabu ya Chelsea ambayo inaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 52 inatarajiwa kuingia kwenye mchezo kwa nguvu katika kutafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kujikita kileleni na kujitengenezea mazingira mazuri ya kunyakua ubingwa.
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho kwenye mchezo huo atamkosa mshambuliaji wake mahiri Diego Costa ambaye ataanza kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu, pia Andre Schurrle na Mohamed Salah ambako wako njiani kuiacha klabu hiyo wanaweza kukosekana kwenye mchezo huo.
Wakati huo huo Cesc Fabregas, Filipe Luis na Branslav Ivanovic wako kwenye hatihati ya kucheza dhidi ya City baada ya wachezaji hao kuumia kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili ya kombe la Capital One dhidi ya Liverpool mapema wiki hii.
Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha klabu ya Chelsea imeshinda michezo 11 na kupoteza mchezo mmoja tu katika michezo 16 iliyopita dhidi ya Manchester City kwenye uwanja wa Stamford Bridge. Pia takwimu zinaonyesha kocha wa Chelsea Jose Mourinho katika michezo 11 kama meneja dhidi ya Manuel Pellegrini ameshinda michezo saba na kufungwa michezo miwili huku akitoka sare michezo miwili.
Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Azpilicueta; Mikel, Matic; Willian, Oscar, Hazard; Drogba
Kwa upande wa Manchester City ambao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 47, alama tano nyuma ya Chelsea wanatarajiwa kucheza kufa na kupona ili kupata ushindi kwenye mchezo huo na kuweza kupunguza tofauti hiyo ya alama tano dhidi ya Chelsea.
Kocha wa Manchetser City Manuel Pellegrini kwenye mchezo huo atawakosa Yaya Toure na Wilfried Bony ambao wanaiwakilisha timu ya taifa ya Ivory Coast kwenye michuano ya AFCON, kiungo Samir Nasri anaweza kucheza mchezo huo baada ya kukosekana kwenye michezo miwili iliyopita kutokana na kuwa majeruhi huku mlinzi Eliaquim Mangala ambaye ana matatizo ya bega ataangaliwa kama anaweza kucheza mchezo huo.
Kuelekea mchezo takwimu zinaonyesha timu ya Manchester City katika michezo minane iliyopita dhidi ya Chelsea imefungwa michezo minne na kushida michezo miwili huku ikitoka sare michezo miwili pia takwimu zinaonyesha Chelsea imeifunga City mara nyingi zaidi mara 22 sawa sawa na Arsenal kuliko timu nyingine yoyote.
Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Kompany, Demichelis, Clichy; Fernandinho, Fernando; Silva, Lampard, Navas; Aguero
0 comments:
Post a Comment