Uchambuzi: Azam fc vs KCCA Mapinduzi Cup.
Na Oscar Oscar Jr
Mabingwa watetezi Tanzania bara timu ya Azam leo watashuka dimbani kupambana na Mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uganda, timu ya KCC kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la Mapinduzi ambalo lilianza kutimua vumbi hapo jana kwa michezo mitatu kupigwa.
Klabu hizo ambazo wiki chache zilizopita walikutana kwenye mchezo wa kirafiki na KCC kufanikiwa kuwalaza Azam kwa mabao 2-0 mabao yakifungwa na Herman Wasswa na mshambuliaji wa zamani wa Azam, Brian Umony wataingia dimbani leo hii wakiwa na lengo la kutetea ubingwa wao.
Tatizo pekee ambalo linatofautisha mchezo huo na ule wa kirafiki uliochezwa Kampala Uganda ni kikosi cha KCC kuwakosa wachezaji wake muhimu huku Azam ikimkaribisha nahodha wao, John Bocco.
kwa mujibu wa mtandao wa Kawowo, timu hiyo itamkosa beki wa kati Richard Kasagga ambaye amekwenda kufanya majaribio nchini Lebanon huku Brian Umony, Habib Kavuma na Isaac Ntege wakishindwa kusafiri na timu kutokana na kuwa majeruhi.
Kwa upande wa Azam, wao watamkaribisha rasmi mshambuliaji na Nahodha wa timu hiyo John Bocco ambaye alikosekana kwenye kikosi cha kwanza kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
Tayari mchezaji huyo ambaye ndiye mfungaji bora wa klabu yake wa muda wote, ameonyesha cheche zake baada ya ujio wake wa kwanza kwenye mchezo dhidi ya Yanga kufunga bao la kusawazisha kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya 2-2.
Kwa mara ya kwanza kocha msaidizi wa Azam, George Nsimbe na kiungo mshambuliaji mpya wa Azam, Brian Majwega watakutana na timu yao ya zamani kwenye mchezo wa ushindani.
Azam bado hawaonekani kucheza kwa maelewano hasa kwenye safu ya ulinzi ambako kocha Joseph Omog ameonyesha kuwaanzisha Pascal Wawa na Agrey Moris huku Mwadini Ally akianza golini.
Ukitazama mchezo wao dhidi ya Yanga na aina ya magoli waliyofungwa, bado utagundua kuwa Wawa bado hajarudi kwenye ubora wake na hata kipa Mwadini Ally amekuwa na maamuzi ambayo sio sahihi kitu kinachopeleka kuruhusu mabao mepesi.
KCC ambao wanakamata nafasi ya tatu ligi kuu nchini Uganda baada ya michezo 15, wameshafungwa michezo mitatu na kutoka sare mara tatu huku michezo tisa yote wakiibuka na ushindi.
Tofauti yao na vinara wa ligi hiyo timu ya Vipers ni alama tano pekee ambapo KCC wana alama 30 huku Vipers wakiwa na 35.
Kwa upande wa Azam, wao pia wanashika nafasi ya tatu baada ya michezo nane, wameshafungwa michezo miwili na kutoka sare mara mbili huku wakishinda michezo minne.
Didier Kavumbagu ndiye kinara wa mabao wa ligi kuu akiwa na mabao matano na leo hii atakuwa akiongoza safu ya ushambuliji ambapo anaweza kuungana na Kipre-Tchetche au John Bocco ambaye amepona kabisa.
Ukitazama lengo la makocha wote wa timu hizi, ni kuhakikisha wanafanya vizuri na kuitumia michuano hii kama sehemu ya maandalizi kueleka michuano ya klabu bingwa Afrika ambapo timu hizi zote zinashiriki.
0 comments:
Post a Comment