Prisons vs Ndanda: Sokoine Stadium.
Na Oscar Oscar Jr
Ligi kuu Tanzania bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja ambao unatarajiwa kupigwa kwenye dimba la Sokoine Jijini Mbeya kwa kuzikutanisha Tanzania Prisons ambao wanakamata nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi kuu dhidi ya Ndanda Fc ambao wanakamata nafasi ya 14.
Msisimko wa mechi hii unakuja pale ambapo kila timu inataka kujinasua na maeneo ya kushuka daraja huku matokeo ya mechi zilizopita pia hayakuwa mazuri kwa timu zote mbili baada ya Ndanda kuchezea kichapo cha bao 1-0 mbele ya Mbeya City huku Prisons wao wakitoka sare ya bila kufungana na Coastal Union.
Ndanda bado wanaonekana ni timu ambayo haiko vizuri hasa kwenye safu yao ya Ulinzi na hii imewafanya kuruhusu mpaka sasa mabao 14.
Ndanda wamekuwa na tatizo la mipira ya adhabu (Set Pieces) ambayo imechangia nusu ya magoli waliyofungwa yapatikane na hivyo kocha Abdul Mingange wa Ndanda Fc atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha mipira hiyo wanaiepuka kwenye mchezo wa leo.
Baada ya mchezo wa leo, Ndanda watafunga safari na kurudi nyumbani Mtwara kuwasubiri Polis Morogoro kwenye mchezo wa mzunguko wa 10 huku Tanzania Prisons, wao watakwenda Morogoro kuvaana na vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar ambao kwa sasa wapo Zanzibar wakishiriki michuano ya Mapinduzi.
0 comments:
Post a Comment