Coastal Union wachezea kichapo leo.
Na Oscar Oscar Jr
Ligi kuu Tanzania bara imeendelea leo kwenye viwanja vitatu hapa nchini ambapo Coastal Union wakiwa nyumbani kwenye dimba la Mkwakwani wamekubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Maafande wa Ruvu JKT bao hilo likifungwa kipindi cha kwanza.
Coastal Union ambao walikuwa na alama 12 huku wakishika nafasi ya tano, wamejikuta wakikubali kichapo hicho cha tatu kwa msimu huu na hivyo kuanza kuonyesha ishara mbaya kwa kocha James Nandwa.
Nandwa ambaye amekuja kuchukuwa nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Yusuph Chippo aliyetimkia klabu ya AFC Leopards ya nchini Kenya aliingoza timu hiyo wiki iliyopita kutoka sare na Tanzania Prisons mkoani Mbeya.
JKT Ruvu baada ya kupoteza mchezo wao uliopita mbele ya majirani zao timu ya Ruvu Shooting, wamejipatia ushindi huo ambao umewafanya sasa kutimiza alama 13 na sasa kuondoa presha kabisa kwa kocha wa kikosi hicho Felix Minziro.
Mechi inayofuata, Coastal Union wataendelea kubakia nyumbani Tanga na awamu hii watawakaribisha wana Jangwani timu ya Yanga na baada ya hapo, watawaalika maafande wa Polis Moro kwenye mchezo wa mzunguko wa 11.
Kwa upande wa Ruvu JKT, wao watarejea nyumbani kwenye dimba la Azam Complex kucheza na Stand United na baada ya hapo kwenye mzunguko wa 11 watakipiga kwenye dimba hilo na Mtibwa Sugar kutoka Manungu kule mkoani Morogoro.
0 comments:
Post a Comment