Na Chikoti Cico
Ligi kuu ya nchini Uingereza itaendelea kushika kasi kwenye viwanja mbalimbali siku ya Jumapili na katika uwanja wa White Hart Lane, Tottenham Hotspur itaikaribisha timu ya Manchester United katika mchezo ambao utaanza mida ya saa 9 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.
Spurs baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Leicester City kwa magoli 2-1 matokeo yaliyopelekea timu hiyo kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 30 sawa na wapinzani wao timu ya Arsenal ambao wanashika nafasi ya tano wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo wakiwa na ari kubwa ya kushinda.
Kocha wa Spurs Mauricio Pochettino kuelekea mchezo huo atakuwa na kikosi kamili huku kukiwa hakuna mchezaji aliye majeruhi, kipa wa timu hiyo Hugo Lloris ambaye aliumia mdomoni kwenye mchezo dhidi ya Leicester anaendelea vyema na yuko fiti kuikabili United.
Kuelekea mchezo pamoja na kuwa nyumbani Spurs wamekuwa na takwimu mbaya kwenye uwanja wao wa White Hart Lane dhidi ya Manchester kwani katika michezo 13 iliyopita dhidi ya United kwenye uwanja huo wamefungwa michezo minane na kutoka sare michezo mitano huku wakiwa hawajashinda hata mchezo mmoja.
Kikosi cha Pochettino kinaweza kuwa hivi: Lloris; Walker, Fazio, Vertonghen, Davies; Mason, Bentaleb; Chadli, Eriksen, Lamela; Kane
Nao Manchester United baada ya kuifunga timu ya Newcastle United kwa magoli 3-1 na kuendelea kubaki kwenye nafasi ya tatu ndani ya msimamo wa ligi huku wakiwa na alama 35 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo kwa nguvu zote huku wakitafuta alama tatu muhimu ili kuendelea kujikita kileleni.
Kocha wa Manchester United Louis van Gaal kuelekea mchezo huo atawakosa Marouane Fellaini, Adnan Januzaj, Daley Blind, Marcos Rojo na Ander Herrera ambao ni majeruhi huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa kucheza kwa kiungo Angel di Maria ambaye alipata majeraha mazoezini.
Kuelekea mchezo huo mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney anaonekana kuwa na rekodi nzuri ya magoli dhidi ya Spurs kwani katika michezo 13 aliyocheza dhidi yao amefunga jumla ya magoli tisa na magoli sita kati ya hayo ameyafunga kwenye uwanja wa White Hart Lane.
Pia Manchester United inaonekana kuwa na rekodi nzuri kwenye mji wa London kwani katika michezo 18 iliyopita ya ligi iliyocheza jijini hapo imeshinda michezo 11 huku ikifungwa mchezo mmoja na kutoka sare michezo sita.
Kikosi cha Van Gaal kinaweza kuwa hivi: De Gea; Jones, Smalling, Evans; Valencia, Carrick, Rooney, Young; Mata; Van Persie, Wilson
0 comments:
Post a Comment