Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 December 2014
Sunday, December 28, 2014

Uchambuzi: West Ham United vs Arsenal


Na Chikoti Cico

Ndani ya uwanja wa Upton Park wenyeji timu ya West Ham United wataialika timu ya Arsenal kwenye moja ya mechi za ligi kuu nchini Uingereza mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa ligi hiyo.

West Ham baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Chelsea ambapo walifungwa kwa magoli 2-0, matokeo yaliyopeleka timu hiyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi huku wakiwa na alama 31wanatarajiwa kupigana kufa na kupona ili kutafuta alama tatu muhimu na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia “top four”.

Kuelekea mchezo huo kocha wa West Ham Sam Allardyce ataendelea kumkosa beki wake James Tomkins ambaye ni majeruhi hivyo James Collins ataendelea kucheza kwenye nafasi ya ulinzi huku pia Alex Song na Diafra Sakho wakitarajiwa kuanza kwenye mchezo huo baada ya kuanzia benchi kwenye mchezo uliopita dhidi ya Chelsea.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha timu ya West Ham wamekuwa na rekodi mbovu dhidi ya Arsenal kwani katika michezo 12 iliyopita ya ligi wamefungwa michezo 10 na kutoka sare michezo miwili huku wakiwa hawajashinda mchezo wowote.

Kikosi cha West Ham kinaweza kuwa hivi: Adrian; Jenkinson, Collins, Reid, Cresswell; Nolan, Song, Kouyate, Downing; Sakho, Carroll

Kwa upande wa Arsenal mshambuliaji wa timu hiyo Olivier Giroud ataanza kutumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya QPR.

 Aaron Ramsey, Mikel Arteta, Mesut Ozil, Abou Diaby, Jack Wilshere na Serge Gnabry ambao ni majeruhi watakosekana kwenye mchezo huo huku beki wa katikati Laurent Koscielny akitarajiwa kurejea kikosini.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger kuelekea mchezo anatarajiwa kuhakikisha timu yake inapata ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kurejea “top four” kwani mpaka sasa washika bunduki hao wa jiji la London wanashika nafasi ya sita wakiwa na alama 30.

Winga wa Arsenal Theo Walcott anaonekana kuwa na rekodi nzuri ya magoli dhidi ya West Ham kwani katika michezo minne iliyopita aliyocheza dhidi yao amefunga jumla ya magoli matano.

Pia mshambuliaji wa timu hiyo Lucas Podolski naye pia akifunga jumla ya magoli manne katika michezo minne aliyocheza dhidi ya West Ham.

Pia timu ya Arsenal inaonekana kuwa na rekodi nzuri kwenye uwanja wa Upton Park dhidi ya West Ham huku ikiwa ni timu iliyoshinda mara nyingi zaidi kwenye uwanja huo, imeshinda mara 10.

Kikosi cha Arsenal kinaweza kuwa hivi: Szczesny; Debuchy, Mertesacker, Koscielny, Gibbs; Rosicky, Flamini, Cazorla; Oxlade-Chamberlain, Welbeck, Sanchez

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!