Simba watoa neno kuhusu Patrick Phiri.
Na Oscar Oscar Jr
Timu ya Simba ambayo inakamata nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara inajiandaa kuondoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar keshokutwa kushiriki michuano ya Mapinduzi ambayo itaanza mapema mwezi Januari.
Akizungumza na kituo cha Redio cha E-FM, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu amethibitisha timu hiyo kushiriki kwenye michuano hiyo huku akibainisha kuwa wapo tayari kupeleka kikosi kamili kuhakikisha kuwa wanafanya vema.
Michuano hiyo inakuja kuharibu ratiba ya Ligi kuu Tanzania bara kwani Simba wanatakiwa kucheza na Mgambo Shooting mwishoni mwa juma hili kwenye dimba la Mkwakwani Jijini Tanga lakini kutokana na kushiriki michuano hiyo, ratiba hilo italazimika kuahirishwa.
Alipoulizwa juu ya kuwepo kwa taarifa za kocha mkuu wa timu hiyo Patrick Phiri kukalia kuti kavu, Kaburu amesema madai hayo sio ya kweli na mpaka sasa bado Phiri ndiye kocha mkuu wa timu hiyo na kama kutakuwa na mabadiliko yoyote hawatasita kuwajulisha wananchi.
Kumekuwa na taarifa za kocha wa timu hiyo kuwa njia panda kufuatia matokeo mabovu ambayo ameyapata mpaka sasa ambapo, katika mechi nane wameshinda mchezo mmoja tu huku wakitoka sare mara sita na kuchezea kichapo mara moja.
Katika kipindi cha usajili kilichofungwa hivi karibuni, Simba wameongeza nguvu ya wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi huku matarajio ya wanachama na viongozi yakiwa makubwa pengine kuliko uhalisia.
Baada ya kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, viongozi wanaonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo na dalili zinazoashiria kocha huyo hana maisha marefu kwenye klabu hiyo.
0 comments:
Post a Comment