Angalau soka la Yanga limeanza kurejea.
Na Samuel Samuel
0652464525
Kama unataka kushuhudia mpira wa visasi , kukamiana na kila aina ya vituko basi subiri mechi ya za watani wa jadi Simba na Yanga lakini ukitaka kujua tathimini ya kukua kwa soka la Tanzania njoo zinapokutana Yanga SC na Azam FC .
Mchezo wa Yanga dhidi ya Azam umemalizika jioni ya leo katika dimba la Taifa Dar es Salaam kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2. Didier Kavumbagu na John Bocco walifunga magoli ya Azam huku yale ya Yanga yakifungwa na Amisi Tambwe na Simoni Msuva.
Timu zinacheza bila pressure na kwa amani kabisa. kocha mkuu wa Dar young African, Hans Van Der Pluijm amedhihirisha yeye ni fundi wa soka safi na la kuvutia.
Hii si Yanga ya Maximo iliyokuwa ikicheza kwenye minyororo ya kujilinda zaidi. Amepanga kikosi cha ushindi na toka mwanzo wachezaji walionesha ari na moyo wa kusaka ushindi.
Yanga wanapaswa kujilaumu yenyewe kushindwa kuondoka na pointi tatu uwanja wa Taifa. Hans hakupaswa kuwapanga Mrwanda na Manyama pamoja.
Kipindi chote cha kwanza wing ya kushoto ya Yanga imeonesha udhaifu mkubwa na kupeelekea kuigharimu timu. Manyama jezi namba 28 mgongoni alionesha udhaifu mkubwa wa kukaba na kuondosha hatari langoni lakini pia Mrwanda kiasilia si mkabaji.
Alishindwa kabisa kumsaidia Manyama kama walivyokuwa wakifanya Msuva na Juma Abduli. Azam baada ya kuiona kasi ya Yanga basi walijipanga vizuri kutumia makosa ya Yanga hasa safu ya ulinzi na kuwaadhibu.
Azam FC imeonesha nidhamu nzuri ya kutulia na kutumia makosa ya Yanga kujinasua kufungwa . Lakini lingine backline ya Yanga lazima ijifunze kujiamini kama Nadir anakosekana kwenye safu ya ulinzi.
Yondani amekuwa na makosa mengi na Dida bado anafanya makosa yale ya kutojua wakati gani atoke, kuzungumza na beki na juhudi binafsi hasa mipira ya juu.
John Bocco aliyesawazisha goli ni kama ametuma salamu za kujiangalia kwa beki ya Yanga. Kwa jinsi Yanga ilivyokuwa na kiu ya kuendelea kufunga basi droo hii ni kama ushindi kwa pande zote mbili.
Kabla ya mechi hii, timu hizi msimu uliopita Azam FC aliifunga Yanga 3-2 na baadaye walikwenda sare ya 1-1 zote zikiwa mechi za ligi msimu wa 2013-14. Mechi ya mwisho ni kwenye Ngao ya jamii Yanga ikilipa kisasi kwa kuibamiza Azam FC 3-0.
0 comments:
Post a Comment