Kuelekea: Prisons vs Coastal Union
Na Oscar Oscar Jr
Katika dimba la Sokoine jijini Mbeya, leo hii utapigwa mchezo mmoja ambapo Tanzania Prisons watawakaribisha Coastal Union kwenye mzunguko wa nane wa ligi kuu Tanzania bara.
Tanzania Prisons ndiyo timu inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo kwa timu za majeshi ikifuatiwa na Ruvu Shooting.
Prisons tayari wameshapoteza mechi tatu na kupata ushindi kwenye mchezo mmoja tu tangu kuanza kwa ligi kuu msimu huu.
Kocha David Mwamwaja anakibarua kigumu cha kuhakikisha vijana wake leo wanapata ushindi mbele ya Coastal Union ambao wanakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kuu.
Kwa upande wa Coastal Union ambao wametoka kumpoteza kocha wao mkuu bwana Yusuph Chippo huku mikoba yake ikichukuliwa na James Nandwa, wanaonekana imara zaidi kwenye safu yao ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa wameshafunga mabao tisa na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba.
Coastal Union ambayo imeonekana kuimarika msimu huu wamekuwa hawana rekodi nzuri sana wanapocheza kwenye dimba la Sokoine ambapo msimu tayari walipoteza mchezo wao wa awali waliocheza dhidi ya Mbeya City na leo pengine ni fursa kwao ya kuanza kupata ushindi.
Endapo Coastal Union wataibuka na ushindi, watatimiza alama 14 ambazo zitakuwa zinaendelea kuwaweka kwenye kundi la timu zinazogombea nafasi mbili za juu.
Tanzania Prisons kwa upande wao, watakuwa wanataka kuondoa upepo mbaya ambao msimu uliopita walikaribia kushuka daraja na hivyo watahitaji alama tatu ambazo zitawafanya watimize alama tisa na kujinasua kwenye zile timu tatu za chini.
0 comments:
Post a Comment