Na Chikoti Cico
Chelsea wako vizuri, Chelsea inapendeza kuwatazama ndivyo unavyoweza kusema baada ya mchezo wa jana dhidi ya West Ham kwenye uwanja wa Stamford Bridge ambapo Chelsea iliibuka kidedea kwa ushindi wa magoli 2-0.
Toka kuanza kwa mchezo Chelsea walionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku kiungo mahiri wa Chelsea Cesc Fabregas akiwa kiini cha mchezo wa pasi nyingi maarufu kama “sexy football” ulioonyeshwa na Chelsea siku ya jana.
Baada ya kulishambulia lango la West Ham kwa muda mrefu kupitia kwa Eden Hazard, Willian an Diego Costa Chelsea ilifanikiwa kupata goli la kuongoza kwenye dakika ya 31 kupitia kwa nahodha wao John Terry aliyeunganisha mpira wa kona ulioguswa kwa kichwa na Costa kabla ya kuusukumiza wavuni.
Baada ya goli hilo Chelsea waliendelea kuliandama goli la West Ham maarufu kama “wagonga nyundo wa London” huku kipa wa timu hiyo Adrian akizuia michomo mingi na mpaka timu zinaenda mapumziko Chelsea walikuwa mbele kwa goli moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Chelsea wakiendelea kutawala mchezo huo huku West Ham muda mrefu wakikabia karibu na lango lao na kuwaacha Fabregas na Matic wakitawala eneo la katikati ya uwanja.
Kuingia kwa Song na Sakho kuliiongezea nguvu timu ya West Ham kwenye eneo la kiungo lakini dakika ya 62 Chelsea kupitia kwa Diego Costa waliandika bao la pili baada ya mshambuliaji huyo kupokea pasi kutoka kwa Hazard kabla ya kuwahadaa mabeki wa West Ham na kuachia shuti kali kwa mguu wa kushoto lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Baada ya goli hilo la pili West Ham walijitahidi kutafuta nafasi ya kupata hata goli la kufutia machozi lakini ubora wa beki ya Chelsea uliwazuia vijana hao wa Sam Allardyce kupata goli lolote.
Mpira ukielekea kumalizika Chelsea waliwaingiza Drogba, Mikel na Ramirez huku West Ham wakimwingiza Amalfitano mabadiliko ambayo hayakuzaa matunda kwa timu zote mbili huku Chelsea wakilinda zaidi magoli yao mawili.
Wachezaji wa West Ham Collins, Cresswell na Reid walionyeshwa kadi za njano na mwamuzi wa mchezo huo Michael Oliver na mpaka mwamuzi anapuliza kipenga kumaliza mchezo huo Chelsea waliondoka uwanjani kifua mbele na hivyo kuwapa mashabiki wao zawadi ya Krismasi.
0 comments:
Post a Comment