Mbaya wa Yanga, kocha mkuu Uholanzi.
Na Oscar Oscar Jr
Ukisema wa nini, wenzio wanasema watampata lini. Huu ni msemo wa zamani kidogo wa mtaani hasa hapa kwetu Tanzania. Ndicho ambacho unaweza kuzungumza hasa unapozitazama timu zetu kubwa za Simba na Yanga kwa namna zinavyoajiri na kutimua makocha.
Aliyekuwa kocha wa Yanga, Muholanzi Ernie Brandts ambaye aliwapa Yanga ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2012/2013 na baadaye kutimuliwa kutokana na kutoka sare kwenye mchezo wa kirafiki maarufu kwa jina la Mtani Jembe dhidi ya watani zao timu ya Simba, kwa sasa ni kocha mkuu nchini Uholanzi.
Brants ambaye pia amewahi kucheza mpira wa kimataifa na kushiriki kombe la dunia wakati akiwa kijana, mwaka huu alikabidhiwa mikoba ya kuiongoza timu ya Dordrecht ambayo inashiriki ligi kuu ya nchini Uholanzi maarufu kwa jina la Eradivisie.
Pamoja na kuwa timu hiyo inaonekana kutofanya vizuri kwenye ligi kuu ya nchini humo ambapo inakama nafasi ya mwisho, bado kitendo tu cha kupewa klabu ya ligi kuu ni ishara tosha kuwa kocha huyo alikuwa na ubora unaostahili kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kufanya kazi nchini Tanzania.
Makocha wengi wanaokuja Tanzania, mara nyingi wamekuwa ni watu wenye CV zao nzuri tu lakini kitendo cha viongozi wetu kujifanya wajuaji sana na kukosa uvumilivu limekuwa ni tatizo ambalo linawafanya makocha hao wenye ubora kushindwa kudumu kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment