Manchester United yapunguzwa kasi.
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya kushinda mechi sita mfululizo, kikosi cha Manchester United kilijikuta kwenye hali ngumu hapo jana mbele ya Aston Vston Villa na kuambulia sare ya 1-1 huku Manchester United wakiwa na kazi ya kusawazisha baada ya mshambuliaji, Christian Benteke kufunga bao la kutangulia.
Manchester United ambayo ilianza na washambuliaji Radamel Falcao na Roben Van Persie huku Wayne Rooney na Darren Fletcher wakianza sehemu ya kiungo, ilijikuta kwenye hali ngumu na kushindwa kuipenya ngome ya Aston Villa ambayo jana ilikuwa na walinzi watano baada ya kocha Paul Lambert kuamua kuwaanzisha walinzi wa tatu eneo la kati.
Mchezo huo ulishuhudia kadi nyekundu yenye utata ambapo mshambuliaji wa kutumainiwa wa Aston Villa, Gabriel Agbonlahor alionyesha kadi hiyo baada ya kugongana na Ashley Young wakati wakigombea mpira. Pamoja na kadi hiyo bado Manchester United hawakuonekana kunufaika na wachezaji wa Aston Villa kuwa pungufu.
Matokeo hayo yanaendelea kuwabakisha Manchester United kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi 32 huku West Ham wakisalia kwenye nafasi ya nne baada ya hapo jana kushinda na kufikisha alama 31.
Katika mchezo huo, Radamel Falcao ndiye aliyefunga goli la kusawazisha na kuwa bao lake la pili kuifungia Manchester United tangu alipojiunga kwa mkopo akitokea klabu ya Monaco ya nchini Ufaransa.
Mchezaji bora wa mwaka wa Argentina, Angel Di Maria naye aliweza kuingia kipindi cha pili na kuchukuwa nafasi ya Roben Van Persie ingawa bado mchezaji huyo anaonekana kutokuwa kwenye ubora wake kufuatia majeruhi ambayo yalimuweka nje kwa muda.
Kasi ya Andreas Weinman na Carlos Sanchez wa Aston Villa, iliendelea kuonyesha mapungufu ya Manchester United huku Fabian Delph akionekana kuivuruga safu ya ulinzi ya vijana wa kocha Loius Van Gaal ambayo ilikuwa inaongozwa na Phil Jones.
Ashley Young alikuwa kwenye kiwango kizuri na kupiga krosi ambayo iliunganishwa moja kwa moja na Falcao katika goli la kusawazisha ingawa kitendo cha kujiangusha na kupelekea kadi nyekundu kwa Agbonlahor, kilifanya mashabiki kumzomea muda wote.
Leo kuna mechi mbili ambazo zitapigwa huku Newcastle United wakiwa St. James's Park kuwakaribisha Sunderland majira ya saa 10:30 Jioni na baadaye majira ya saa 1:00 Usiku, kutakuwa na mpambano ndani ya dimba la Anfield ambapo majogoo wa jiji timu ya Liverpool itawakaribisha vijana wa Arsene Wenger timu ya Arsenal.
0 comments:
Post a Comment